Oparesheni ya kutumbua majipu imetua katika Jeshi la Polisi ambapo Mkuu wa Kituo cha Himo (OCS), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Zuhura Suleiman pamoja na koplo Federika Shirima wamekumbwa na panga hilo baada ya kukutwa na magari ya wizi.

Jeshi hilo limemvua cheo mkuu huyo wa kituo cha polisi baada ya kumkuta na gari aina ya Toyota Rav4 lililobainika kuwa ni la wizi. Aidha, limemfukuza kazi koplo Shirima baada ya kujiridhisha kuwa alikutwa na magari mawili yaliyoibwa jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Mwananchi, chanzo chake kilieleza kuwa koplo huyo alisomewa barua ya kuachishwa kazi juzi, tofauti na OCS ambaye ana vyeo viwili na kwamba mwenye mamlaka ya kumvua cheo cha ASP ni Katibu Mkuu wa wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

”Kwa cheo cha ASP mamlaka yake mamlaka yake ya nidhamu ni Katibu Mkuu, kwa hiyo kilichofanyika kwahiyo kilichofanyika ni kumuondoa kwenye wadhfa wa OCS akisubiri uamuzi mwingine kutoka juu,” gazeti hilo limekikariri chanzo chake.

Dar24 imefanya jitihada za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa lakini amekuwa akikata simu kutokana na hali inayoonesha huenda yuko katika majukumu mengine ambayo hawezi kuzungumza na simu.

Martin Glenn: Michezo Ya PL Itaendelea Mwishoni Mwa Mwaka
Bilionea amtosa Mariah Carey kwa kupenda 'vya bei kali na starehe’