Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amesema hatashangaa rais wa sasa, Dk John Pombe Magufuli kwenda Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumamosi kushuhudia mchezo dhidi ya Algeria.

Tanzania, ‘Taifa Stars’ itamenyana na Algeria, ‘Mbweha wa Jangwani’ Jumamosi kabla ya kurudiana Novemba 17 mjini Algiers na mshindi wa jumla ataingia kwenye makundi ya kuwania tiketi ya Kombe la Dunia 2018 Urusi.

Na akizungumza nyumbani kwake, Msoga, Bagamoyo mkoani Pwani, Rais mstaafu Kikwete amesema hatashangaa Rais wa sasa, Dk Magufuli akienda kushuhudia mchezo huo, kwa sababu naye ni mpenzi wa michezo.

“Sitashangaa hata rais wetu, Dk John Pombe Magufuli akienda kuongoza Watanzania kuishangilia Taifa Stars, maana naye anapenda michezo,”alisema Kikwete jana akizungumza na Ujumbe wa Kamati ya Taifa Stars uliomtembelea nyumbani kwake.

Akiuzungumzia mchezo huo, Dk Kikwete amesema kwamba anaamini Taifa Stars inaweza kuifunga Algeria japokuwa ndiyo bora kwa sasa Afrika, kikubwa ni uteuzi wa wachezaji bora na maandalizi mazuri.

“Wahenga wana msemo wao mmoja kwamba, Hata bahari kubwa huvukwa, basi nami naamini tunaweza kuifunga Algeria, kikubwa watu wajitokeze kwa wingi kuisapoti timu Jumamosi, kwa sababu shabiki ni mchezaji wa 12,”amesema Rais Kikwete.

Dk Kikwete aliyeondoka madarakani rasmi Novemba 5, mwaka huu baada ya kuiongoza Tanzania kwa miaka 10, akimrithi Benjamin William Mkapa, amesema katika kusaidia kampeni ya Taifa Stars dhidi ya Algeria naye atatoa mchango wake.

“Nami nitachangia, lakini si kwa kiwango kikubwa, kwa sababu mimi sasa hivi ni mstaafu, naishi kwa pensheni. Nilipokuwa madarakani nilisaidia sana na nilihamasisha watu kuipenda timu yao ya taifa, nilivaa hadi jezi za timu ya taifa ili kuwashawishi watu kuipenda timu yao,”

“Maana wakati huo hali ilikuwa mbaya sana, watu walikuwa wanapenda klabu zao tu, hata wachezaji walikuwa hawataki kuchezea timu ya taifa, lakini tukafanikiwa kuwarudisha na sasa imefikia mchezaji asipoteuliwa Taifa Stars anaumia, hata klabu zinapenda wachezaji wao waitwe timu ya taifa,”alisema Dk. Kikwete.

Rais huyo mstaafu amewaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi Jumamosi Uwanja wa Taifa, kushangilia Taifa Stars ili kuwatia nguvu na hamasa wachezaji wawafunge Algeria.

Mabalaa Yaendelea Kuishukia Chelsea
Bartomeu Akiri Kumuhitaji Messi Game Ya Nov 21