Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake amesema pato la Taifa limekua kwa asilimia 7.0 mwaka 2019, kama ilivyokuwa mwaka 2018.
Ameeleza Sekta zilizokuwa na mchango mkubwa katika Pato la Taifa kwa mwaka 2019 ni Kilimo (26.6%); Ujenzi (14.3%); Biashara na Matengenezo (8.8%); Viwanda (8.5%) na Usafirishaji na Uhifadhi mizigo (6.9%).
Sekta zilizoongoza katika ukuaji ni pamoja na Uchimbaji wa Madini na Mawe 17.7%, Ujenzi, 14.1%, Sanaa na Burudani 11.2% na Usafirishaji na Uhifadhi wa Mizigo 8.7%.
Pia, Waziri Dkt. Mpango amebainisha kuwa mfumuko wa bei umeendelea kubaki katika wigo wa tarakimu moja ambapo kwa mwezi Machi 2020, ulikuwa asilimia 3.4.
Aidha, amesema kutokana na uchambuzi wa awali, shabaha za uchumi jumla katika mwaka 2020/21 ni Pato halisi la Taifa linatarajiwa kukua kwa 4.0% mwaka 2020; mapato ya ndani 14.5% ya Pato la Taifa; na mapato ya kodi 12.5% ya Pato la Taifa.