Serikali inatarajia kumega hekta 10,828 kutoka katika msitu wa hifadhi wa Loasi, kwa ajili ya shughuli za kilimo, ufugaji na makazi za Wananchi wa Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa.
Kauli hiyo, imetolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja wakati akijibu swali la Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Aida Khenani kuhusu mkakati wa serikali wa kuwapatia wananchi maeneo ya kulima kutoka kwenye mapori na hifadhi zisizo na wanyama.
Amesema, Wilaya ya Nkasi inatakiwa kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kukidhi mahitaji ya wananchi kwani Wilaya ina changamoto ya mgawanyo na mtawanyiko wa makazi na shughuli za kibinadamu.
Naibu Waziri Masanja, pia amekemea tabia ya baadhi ya wananchi kuvamia maeneo ya hifadhi na kujichukulia sheria mkononi ya kuwadhuru wahifadhi.