Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli amempongeza Jaji Zephrine Galeba wa Mahakama Kuu ya Kanda ya Musoma kwa kutoa hukumu ya kesi kwa kutumia lugha ya Kiswahili, ambapo amempandisha cheo na kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Rufaa.
Hayo yamejiri wakati wa maadhimisho ya wiki ya sheria na miaka 100 ya Mahakama kuu yaliyofanyika Chinangali Jijini Dodoma leo Februari 1, 2021, ambapo Rais Magufuli amesema kuwa kutumika kwa Kiswahili ni mwanzo mzuri katika kuenzi lugha ya Kiswahili na kumuona Jaji Galeba kama shujaa katika muhimili wa Mahakama.
“Nampongeza sana Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma kwa kutumia Kiswahili kutoa hukumu kwenye kesi ya North Mara Gold Mine dhidi ya Gerald Nzumbi, ninajua alisemwa sana, amekuwa mzalendo wa kwanza kwa kuandika kwa lugha ya Kiswahili na mimi leo nampandisha cheo kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa kwa uzalendo huo wa kitanzania wa kukwepa miiko iliyopo ndani ya Mahakama”, amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amewasihi wadau wote wa Mahakama ikiwemo Bunge, Wizara ya Katiba na Sheria na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuandaa mkakati wa kuwezesha lugha ya Kiswahili kutumika kwenye maswala ya Sheria na Mahakamani.
Rais Magufuli pia amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini kuhakikisha kamati za maadili zinakutana na kuwasilisha ripoti za mwezi Februari zinazoonyesha ni mara ngapi wamekutana na jinsi walivyotatua changamoto ya kamati hizo.
Sambamba na hilo, Rais Magufuli amesisitiza somo la Historia kuwa somo la lazima kwakuwa kuna baadhi ya watu wananbeza maendeleo yaliyotokana na Uhuru.