Meneja wa klabu ya Everton Ronald Koeman, kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa tayari kumsajili mshambuliaji na nahodha wa Man Utd Wayne Rooney.

Koeman amekua akisisitiza suala la kumsajili Rooney, kutokana na mwenendo wake ndani ya kikosi cha Man utd, kukabiliwa na changamoto za kushindwa kucheza katika kikosi cha kwanza, kwa zaidi ya michezo sita, tangu alipowasili meneja Jose Mourinho.

Koeman amesema hakuna linaloshindikana katika suala la kumsajili Rooney, kutokana na kufamika wazi kuwa mshambuliaji huyo bado ana mapenzi ya dhati ya klabu ya Everton ambayo ilimkuza na kumuendeleza kisoka kabla ya kumruhusu kujiunga na Man Utd mwaka 2004.

Kabla ya ushindi wa mabao mawili kwa sifuri dhidi ya West Ham Utd hapo jana, Koeman aliulizwa na waandishi wa habari kuhusu uwezekano wa kumnusuru mshambuliaji huyo na alijibu: “Sifahamu – lakini tuna matarajio.

“Kama itatokea anahitaji kujiunga na Everton kwa siku zijazo, hatutokua na kipingamizi chochote. Lakini nina uhakika kila mmoja wenu anafahamu Rooney anaipenda Everton.

“Ninaheshimu maamuzi ya Manchester United, pamoja na ya mchezaji mwenyewe, lakini tunamkaribisha wakati wowote kujiunga nasi.”

Issa Hayatou Amshika Mkono Jamal Malinzi CAF
Historia Ya Soka La Wanawake Kuandikwa Kesho