Mshambuliaji wa FC Barcelona, Luis Suarez amerejea kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Uruguay kwa ajili ya mchezo wa kimashindano, baada ya kumaliza adhabu yake ya kufungiwa michezo tisa na shirikisho la soka duniani FIFA.

Suarez, alitajwa kwenye kikosi cha timu ya taifa lake, kwa ajili ya mchezo wa kuwania nafasi ya kushiriki fainali za kombe la dunia za mwaka 2018, na tayari amejiunga na wenzake kambini mjini Montevideo nchini Uruguay.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 29, aliruhusiwa kucheza michezo ya kimataifa ya kirafiki baada ya kushinda rufaa yake ya kufungiwa kwa kipindi cha miezi minane pamoja na kucheza soka kwa michezo tisa, kufuatia kosa la kumng’ata beki wa timu ya taifa ya Italia Giorgio Chiellini, wakati wa fainali za kombe la dunia za mwaka 2014.

Akiwa katika mazoezi ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Brazil utakaochezwa mwishoni mwa juma hili, Suarez ameonekana ni mwenye furaha na wakati wote alionyesha ushirikiano wa kutosha kwa wachezaji wenzake.

Hata hivyo alipata nafasi ya kuzungumza na vyombo vya habari akiwa katika kambi ya timu ya taifa, na kuonyesha kujutia kosa alilolifanya wakati wa fainali za kombe la dunia za mwaka 2014 kwa kung’ata mchezaji wa Italia pamoja na kuushika mpira kwa makusudi wakati wa fainali za kombe la dunia za mwaka 2010 zilizochezwa nchini Afrika kusini.

Luis Suarez akizuia kwa mkono mpira uliokua unaelekea langoni mwa timu ya Uruguay wakati wa mchezo wa robo fainali katika michuano ya kombe la dunia mwaka 2010 dhidi ya Ghana

Suarez alisema hana budi kujutia vitendo hivyo na anaamini vilimuweka katika mazingira mabaya ya kutazamwa kama muhuni, ambaye hakupaswa kurejea tena katika tasnia ya mchezo wa soka, lakini kwa sasa anawashukuru waliomsihi na kumfundisha mwenendo mzuri wa kuepuka majanga kama hayo.

Suarez was given the ban for biting Giorgio ChielliniSuarez akiwa pembeni baada ya kumng’ata beki wa timu ya taifa ya Italia Giorgio Chiellini wakati wa fainali za kombe la dunia za mwaka 2014

“Nilifanya makossa,’ Suarez aliwaambia waandishi wa habari.”Lakini naamni adhabu iliyotolewa dhidi yangu ilikua fundisho japo niliiona kubwa sana, kutokana na kuniweka mbali na timu yangu ya taifa ilipokua ikicheza michezo ya kimashindano.

“Najua kila mmoja nchini hapa alikasirishwa na nilichokifanya, japo walinionyesha kunikubali kama shujaa wao, lakini kwangu nilijua baada ya kujiona mpuuzi ambaye sikupaswa kusamehewa, lakini leo ninazungumza na kila mmoja kwa kuzingatia maadili mema ya kazi yangu.” Aliongeza Suarez ambaye anaongoza katika orodha ya ufungaji wa mabao katika ligi ya nchini Hispania

Katika harakati za kuwania nafasi ya kufuzu kucheza fainali za kombe la dunia za mwaka 2018, kupitia ukanda wa Amerika kusini (CONMEBOL), Uruguay imeshinda michezo yake mitatu kati ya minne na ipo katika nafasi ya pili kwenye msimamo, ikiwa na tofauti ya point tatu dhidi ya Ecuador walio kileleni kwa kufikisha point 12.

Timu Ya Ferrari Yapata Msiba
TFF Waendelea Kusisitiza Hili Lisifanyike