Mazungumzo yanayoendelea kwa usiri visiwani Zanzibar na Tanzania Bara kutafuta muafaka kufuatia tangazo la Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu visiwani humo yameendelea kuibua ripoti nzito tofauti.

Taarifa zinazodaiwa kutolewa na mmoja kati ya maziri waandamizi wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeeleza kuwa vikao viwili vikubwa vilivvyofanyika katika Ikulu ya Dar es Salaam na ile ya Zanzibar Jumamosi na Jumanne wiki hii vimetoa picha inayompa nafasi zaidi Maalim Seif Sharif Hamad kutangazwa mshindi.

Kwa mujibu wa ‘Mawio’, chanzo hicho cha kuaminika, wajumbe wengi wa vikao hivyo wameelezea kuridhia kuwa uchaguzi wa Zanzibar usirudiwe bali aliyeshinda atangazwe ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kujitokeza.

“Washiriki wengi wa mazungumzo yale wanakubaliana na hoja kwamba kurejea Uchaguzi kutaweza kuingiza nchi katika mgogoro na mkubwa zaidi, “mtoa taarifa anakaririwa na gazeti hilo.

Aliongeza kuwa Maalim Seif ameendelea kushikilia msimamo wake wa kukataa kurejewa kwa uchaguzi badala yake anataka Tume imalize kazi yake na kumtangaza mshindi.

” Hapa Zanzibar chama chetu kinaonekana kusalimu amri. Hii inatokana na msimamo mkali uliowekwa na CUF katika mazungumzo yanayoendelea pamoja na msimamo wa Jumuiya za Kimataifa, “anaendelea kukaririwa.

Aliongeza kuwa vikao vya hivi karibuni vilihudhuriwa na Rais John Magufuli,  Jaji Joseph Warioba, Dk. Salim na Balozi Madiga.

Hata hivyo, hivi karibuni Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Vuai Ali Vuai aliiambia Azam TV kuwa chama chake kinaendelea kufanya maandalizi ya kurejewa kwa uchaguzi kwa kuwa uchaguzi uliofanyika ulifutwa na kutangazwa kwenye gazeti la Serikali hivyo kufutwa kwa Uchaguzi huo kupo kisheria.

Mbeya Kuendesha Kozi Ya Makocha
Masaburi Abariki Ubunge wa Kubenea, atakiwa Amlipe Fidia