Aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Ubungo kwa tiketi ya CCM, Dk. Didas Masaburi ameamua kuondoa mahakamani kesi ya kupinga matokeo yaliyompa ushindi Saed Kubenea (Chadema) aliyoifungua Mahakama Kuu.

Dk. Masaburi ambaye jana alikuwa anatarajiwa kuwasilisha maombi ya kupunguziwa gharama ya kesi hiyo alibadili mawazo na kujiengua.

Kupitia wakili wake, Clemence Kihoko, Dk. Masaburi aliiomba mahakama kufuta kesi hiyo lakini pia aliomba asilipe fidia yoyote kwa Kubenea kwa madai kuwa alikuwa bado hajawasilisha nyaraka zozote mahakamani hapo.

Mawakili wanaomtetea Kubenea walikubali ombi la kufutwa kwa kesi hiyo lakini waliiomba mahakama kuamuru Mlalamikaji kulipa fidia kwa kuwa walikuwa wameshaingia gharama za kuandaa nyaraka pamoja na vikao.

Baada ya kusikiliza pande zote mbili, Jaji Lugano aliamua kuwa Dk. Masaburi amlipe Kubenea asilimia 50 ya gharama alizotumia.

Dk. Masaburi alipinga matokeo ya ubunge wa Jimbo la Ubungo mahakamani hapo akidai kuwa Kubenea alitoa rushwa ya jenereta kwenye hospitali ya Mavurunza na ujenzi wa barabara ya Matete.

Pia alidai kuwa Kubenea aliwashawishi wananchi kwa kuwanunulia vifaa vya michezo.

Dk. Masaburi ambaye alikuwa Meya wa jiji la Dar es Salaam alimlalamikia msimamizi wa Uchaguzi kwa kukataa kurudia kuhesabu kura pamoja na kutomjulisha tarehe, muda na mahali pa kujumlishia matokeo.

Maalim Seif Kukabidhiwa Mikoba Zanzibar Baada Ya 'Vutankuvute'?
Mwanzilishi wa Chadema Amsifu Magufuli, Amshauri