Rais wa Kenya, William Ruto ametangaza kushuka kwa bei ya unga wa mahindi, ikiwa ni matokeo ya mtikisiko wa mwishoni mwa mwezi Machi kutokana na maandamano ya kupinga mfumuko wa bei na gharama ya maisha.
William Ruto ambaye aliyechaguliwa kuwa kiongozi wa Taifa hilo Agosti 2022 amekuwa akikabiliwa na ukosoaji, hasa baada ya kuondoa ruzuku ya gharama kubwa ya mafuta na unga wa mahindi, ambayo bei yake imeongezeka.
Akitangaza punguzo hilo, Rais Ruto amesema, “najua tuna tatizo na gharama ya maisha. Mwishoni mwa wiki ijayo, bei ya unga (unga wa mahindi) itashuka kutokana na kuwasili kwa unga kutoka nje, hiki ni chakula chetu kikuu lazima tuone naman ya kufanya.”
Kenya ambayo ni kiungo muhimu wa Uchumi Afrika Mashariki, inakabiliwa na mfumuko wa bei unaozidi kuimarika, ambao ulifikia 9.2% katika kipindi cha mwaka mmoja mwezi Februari na bei za vyakula pekee ziliongezeka kwa asilimia 13.3.
Kiongozi mkuu wa upinzani Raila Odinga aliandaa maandamano ya siku tatu, Machi 20, 27 na 30, dhidi ya serikali ya William Ruto, ambayo anaituhumu kuiba kura katika uchaguzi wa urais wa 2022 na kushindwa kudhibiti mlipuko wa gharama ya maisha.
Hata hivyo, mikutano hii ilizua uporaji na makabiliano na polisi katika vitongoji duni katika mji mkuu Nairobi na mji wa Kisumu, ngome ya Odinga magharibi mwa nchi na kusababisha vifo vya watu watatu ambapo baadaye alisitisha maandamano, baada ya Ruto kupendekeza mazungumzo bungeni.