Ili kuhakikisha maboresha ya mazingira ya Wanahabari na upatikanaji wa taarifa nchini katika mazingira yote yanaimarika, Serikali inaendelea na mchakato wa kupitia Sheria, Kanuni na Sera ya Habari upo katika hatua vizuri.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa Serikali na Wadau uliokuwa ukijadili maendeleo endelevu ya Vyombo vya Habari Nchini, uliofanyika jijini Dr es salaam Julai 13, 2022.
“Sheria ya huduma za Habari ya mwaka 2016 ilipotungwa ililenga kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya Habari ikiwemo ajira, maslahi, mazingira ya kazi na wajibu wao, Serikali imetoa nafasi kwa Wanahabari kuleta mbadala wa yale yanayolalamikiwa ili kuyaboresha,” amesema Nape.
Amesema, lengo la mchakato wa maboresho ya Sheria ya Huduma za Habari ni kutunga sheria itakayodumu, ambapo Wizara kwa kushirikiana na wadau tayari wameanza kupitia mambo mbalimbali yanayohusu uhuru wa Vyombo vya Habari na upatikanaji wa Habari nchini.
Waziri Nape ameongeza kuwa, “Tumezungumza kuhusu uhuru wa mazingira ya Wanahabari katika kufanya kazi vizuri pamoja na maslahi yao, haya yote ni mambo ya muhimu katika tasnia hii.”
Awali, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Ofisi ya Dar es Salaam, Michael Toto amesema wataendelea kusaidia Wanahabari na Wafanyakazi wa vyombo vya habari kupitia mpango wa utekelezaji wa Umoja wa Mataifa (UN), kuhusu Usalama wa Wanahabari, ili kuwalinda na uhalifu unaofanywa dhidi yao.
“Katika Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, na kupitia majukwaa mengine ya mazungumzo kama vile Siku ya Redio duniani na Siku ya Kimataifa ya kukomesha uhalifu dhidi ya Waandishi wa Habari sisi tunaheshimu kazi muhimu za vyombo vya habari katika kujenga taasisi na jamii imara,” amefafanua Toto.
Kwa upande wake, Balozi wa Switzerland nchini, Didier Chassot amesema nchi yake imekuwa ikishirikiana na sekta ya vyombo vya habari kwa zaidi ya muongo mmoja na kwamba kwa sasa wanajiandaa kutoa Kitabu cha mwaka cha ripoti ya Ubora wa Vyombo vya Habari kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Naye, Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Gerson Msigwa amesema mkutano huo ni muhimu na unalenga kuboresha uratibu wa hatua za wadau mbalimbali katika kuendeleza maendeleo ya vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza, upatikanaji wa habari na mabadiliko ya kidijitali.
Mpango wa Utekelezaji wa Umoja wa Mataifa kuhusu Usalama wa Waandishi wa Habari na ulinzi wao unalenga kuweka mazingira huru na salama kwa waandishi na wafanyakazi wa vyombo vya habari kwa wakati wote wa salama au wa migogoro kwa nia ya kuimarisha amani, demokrasia na maendeleo duniani kote.
Hata hivyo, ili kuimarisha kinga kwa waandishi wa habari, Mpango wa Utekelezaji wa Umoja wa Mataifa unapendekeza kufanya kazi kwa ushirikiano na serikali, vyombo vya habari, vyama vya kitaaluma na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Ushirikiano huo utalenga kufanya kampeni za kuongeza uelewa juu ya masuala mbalimbali kama vile mikataba ya kimataifa iliyopo, hatari inayoongezeka kutokana na vitisho vinavyojitokeza kwa wanataaluma wa habari, wakiwemo watendaji wasio wa serikali, pamoja na miongozo mbalimbali iliyopo kuhusu usalama wa wanahabari.
Tanzania, kwa muda mrefu sasa Wanahabari wamekuwa na malalamiko juu ya baadhi ya vipengele vinavyopendekezwa na Serikali katika kufanya maboresho ya vifungu vya sheria ya Habari ambavyo vinaonekana kuwa kandamizi, hivyo mpango huu utasaidia kuleta suluhu iwapo mapendekezo ya wana tasnia yataridhiwa.