Kufuatia kifo cha Kasobi Shida, mtoto wa dereva wa Mkuu wa Mkoa wa Mara, aliyepata ajali akiendesha gari la Mkuu wa Mkoa baada ya baba yake kulipaki, madaktari wa hospitali ya mkoa huo wamepata mtihani wa kumpa taarifa za kifo hicho dereva huyo ambaye pia anapatiwa matibabu.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Hosea Bisanda amesema kuwa hali ya Shida Masaba, baba wa marehemu inaendelea vizuri lakini bado ana tatizo la kisaikolojia kwani hulia kila anapomuona mtu anayemfahamu.
“Tunafanya utaratibu wa namna ya kumjulisha juu ya kifo cha kijana wake maana hali yake bado, hivyo inabidi tumpe ushauri wa kisaikolojia kabla ya kupata taarifa hizi mbaya,” Dkt. Bisanda anakaririwa.
Akizungumzia kifo cha Kasobi aliyekuwa na umri wa miaka 26, Dkt. Bisanda alisema kuwa walimpokea Agosti 4, 2019 akiwa na majeraha pamoja na maumivu katika maeneo ya tumbo na kifuani. Walimpatia matibabu na baadaye walimfanyia upasuaji kutokana na kulalamika maumivu ya tumbo.
Alieleza kuwa upasuaji ulienda vizuri na akawa katika hali nzuri, lakini ghafla hali yake ilibadilika tena na akapoteza maisha jana majira ya saa mbili usiku.
Kasobi alipata ajali akiwa anaendesha gari la Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, gari ambalo analiendesha baba yake.
Baada ya ajali hiyo, baba yake alipatwa na mshtuko uliosababisha akimbizwe hospitalini kwa ajili ya matibabu. Alilazwa hospitalini hapo hadi leo.
Kwa mujibu wa dada wa marehemu, Anastazia Shida, mdogo wake alikuwa na leseni ya udereva aliyoipata kutoka Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), lakini hakuwa anaendesha gari hivi karibuni.
Alisema alionana na ndugu yake kabla ya kufariki lakini hakuweza kuelezea mazingira ya ajali hiyo, hali inayomfanya abaki na maswali akitaka kujua hasa nini kilitokea.
Kasobi ambaye ni kijana maarufu katika mji wa Musoma kutokana na kuwa shabiki mkubwa wa mpira wa miguu, kwa mujibu wa dada yake, alipata ajali hiyo Jumapili, Agosti 4, 2019.