Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, George Simbachawene ameupongeza mradi wa utunzaji mazingira kupitia upandaji miti ya mikoko visiwani Zanzibar.

Simbachawene ametoa pongezi hizo Agosti 5, 2019 katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kujitambulisha na kukagua miradi ya Muungano na Mazingira visiwani humo.

Amesema kuwa ameridhishwa kuona namna ambavyo Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ilivyotekeleza mradi huo pamoja na ufadhili kutoka Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP).

“Niwapongeze sana kwa mradi huu mzuri na tunaona matokeo yake umesaidia mawimbi yasije kwa kasi katika eneo hili na kusababisha mmonyoko na tukiamua kufanya kazi kwa pamonja na jamii tunaweza kufanya vizuri,” amesema Simbachawene.

Aidha, Simbachawene ametoa wito kwa wataalam kuangalia namna ya kuibua miradi mingine katika fukwe za mikoa mingine kama Dar es Salaam, Tanga, Lindi na Mtwara ili kusaidia kutunza mazingira.

Katika hatua nyingine amekagua ujenzi wa Kituo cha Afya Kianga katika Wilaya ya Magharibi A Mkoa wa Mjini Magharibi na kuwapongeza wananchi kwa kusimamia mradi huo.

“Nawapongeza sana wananchi hasa kwa kamati hii mmefanya vizuri kusimamia mradi huu wa ujenzi wa kituo cha afya tunaamini udokozi haukuwepo kazi imefanyika fenicha (samani) zipo, vifaa tiba na utendaji kazi mzuri unaendelea kufanyika,” ameongeza Simbachawene

Ole Nasha amtaka mkurugenzi kumlipa mhandisi wa manispaa ya Bukoka
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Agosti 6, 2019