Mbunge wa Mwanga (CCM), Jumanne Maghembe ameilalamikia mitandao ya kijamii na kuionya tabia ya kuwaibia wateja wao pesa pindi wanapojiunga na vifurushi vyao.
Akizungumza hayo ametolea mfano mtandao anaotumia yeye wa Vodacom kuwa umekuwa ukimuibia sana dakika zake pindi anapojiunga vifurushi vyao na amewataka kuacha mara moja tabia hiyo.
Hivyo ameomba serikali kuingilia kati suala hilo ili kuwasaidia wananchi ambao ni wahanga wa wizi huo unaofanywa na mitandao ya kijamii.
”Mitandao ya kijamii kudanganya wateja unanunua muda wa maongezi, unaandika dakika ulizotumia, kama ulikuwa na dakika 200 ukifikisha dakika 45 wanakwambia dakika zako karibu zinakwisha ukipiga tena wanakukatia wanakwambia dakika zako zimekwisha, wizi unatokea sana katika mitandao kwa bahati mbaya mimi kwa experience yangu simu yangu ya vodacom inaniibia sana muda wa maongezi, wakati umefika kwa serikali kuingilia mitandao hii ili isiendelee kuwaibia wananchi, na tumepata nafasi hii kuongea hapa watu wa vodacom wasikie kuwa sio vizuri kutuibia pesa zetu tunazoweka huko” amesema Maghembe.
Hayo yamezungumzwa jana bungeni jijini Dodoma.
Aidha ni kweli kabisa kumekuwa na tabia ambayo mitandao ya simu imekuwa ikifanya kwa wateja wao kuwaibia dakika zao za maongezi jambo ambalo si zuri kwa wateja na mitandao hiyo imekuwa ikifanya jambo hilo kutokana na hali ya ulazima ambayo wateja wanayo ya kutaka kufanya mawasiliano.
Hivyo Serikali ni vyema kulichukua na kuliangalia kwa jicho la tatu suala hilo na kulitatua ili kuwasaidia wananchi ambao wanaumia na wizi huo.