Mvutano kati ya vyama vya siasa vya upinzani vinavyounda Ukawa na maelekezo ya Tume ya Uchaguzi kuhusu tafsiri ya sheria ya uchaguzi kuhusu kukaa umbali usiopungua mita 200 au kutokaa kabisa kwenye eneo la kituo cha kupigia kura baada ya kupiga kura umetinga katika Mahakama Kuu ya Tanzania.

Mpiga kura ambaye pia ni mgombea ubunge wa viti maalum jimbo la Kilombero kwa tiketi ya Chadema, Amy Pascience Kibatala, amefungua kesi Mahakama Kuu chini ya hati ya dharura akiiomba mahakama hiyo kutoa tafsiri ya kifungu cha 104 (1) cha Sheria ya Uchaguzi, sura ya 343 kama ilivyorejewa mwaka 2010.

Kibatala ambaye pia ni mwanasheria, amefungua kesi hiyo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhusu tamko la Tume kuwataka wananchi kurudi nyumbani baada ya kupiga kura, huku vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa vikiwataka wananchi hao kuhakikisha wanakaa umbali wa mita 200 baada ya kupiga kura kwa lengo la kulinda kura zao.

Kupitia Facebook, jana Kibatala ameandika:

Leo, 16th October 2015, tumefungua chini ya hati ya haraka sana (certificate of Extreme urgency) shaui namba 37 la mwaka 2015 katika Mahakama Kuu ya Tanzania (Main Registry) tukiomba Mahama Kuu itoe tafsiri sahihi ya Kifungu cha 104 (1) cha Sheria ya Uchaguzi Tanzania na itamke iwapo wapiga kura na watu wengine wenye shauku wanaruhusiwa au la kukaa KWA UTULIVU umbali unaozidi meter 200 kutoka kituo cha kupigia kura/kufanya majumuisho ya kura.

Tumeiomba Mahakama Kuu itamko iwapo ni halali kwa Rais wa nchi kutoa matamko aliyoyatoa kwa namna ya katazo kwa wapiga kura/raia wengye shauku kukaa KWA UTULIVU umbali usiozidi meters 200 kutoka kituo cha kupigia kura/majumuisho.

Pia tumeiomba Mahakama Kuu itamke iwapo Rais ana mamlaka hayo kisheria kwa kuzingatia Sheria ya Uchaguzi Tanzania.

Tunasubiri taratibu za kimahakama kuhusu shauri tajwa.

 

Kingunge Aeleza ‘Kosa Kubwa’ Linalofanywa Na CCM Kwenye Kampeni Mwaka Huu
Soka La Zanzibar Laanza Kupata Nuru