Aliyekuwa kada mkongwe wa CCM, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru amesema kumuangalia mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa badala ya wananchi ni moja kati ya makosa makubwa yanayofanywa na viongozi wa chama chake hicho cha zamani katika harakati za kampeni za mwaka huu.

Akiongea hivi karibuni katika mahojiano maalum na Azam TV kupitia kipindi cha ‘Funguka’, Mzee Kingunge alieleza kuwa viongozi wa CCM walipaswa kuuona umma mkubwa unaomsapoti mgombea huyo wa Chadema badala ya kujikita katika kumshambulia mgombea huyo.

“Mimi ndio maana nachukia kuona watu wanafikiria kulifanya hili suala ni la Lowassa. Suala hili ni la wananchi, na ndio kosa kubwa wanalofanya viongozi wa sasa wa CCM. Wanamtazama Lowassa badala ya kutazama watu wanaomtaka Lowassa,” alisema.

“Sasa na mtazamo huo naona unaendelea hivyo hivyo, wanasema hili jambo la ‘Lowassa tu’. Tazameni umma unaomfuata Lowassa bila kubebwa kwenye malori, wanatembea wenyewe tena wengine wanakimbia. Sasa nasema, wananchi wana matumaini na huyu mtu, hasa wananchi walio wengi. Kujaribu kuwanyang’anya matumaini yao ni kutoitendea haki nchi,” aliongeza.

Kadhalika, Mzee Kingunge aliongeza kuwa kosa jingine linalofanywa na viongozi wa CCM wa sasa ni kauli wanazozitoa hadharani akidai kuwa ni kauli za udhalilishaji zinazowadhalilisha wao pia. Aliongeza kuwa kauli nyingine huashiria kuwa watashinda hata kwa kuvunja taratibu na sheria za nchi.

Mwanasiasa huyo Mkongwe alieleza kuwa ana imani kubwa na Lowassa kuwa ataleta mabadiliko ya kweli nchini ingawa alikuwa ndani ya CCM kwa muda mrefu, huku akitoa mfano wa utendaji kazi wake wakati alipokuwa Waziri Mkuu.

“Kwanza hakuwa rais, pili alikuwa waziri mkuu…si walimuondoa harakaharaka. Lakini tazama alichokifanya ndani ya miaka miwili, kila mtu anazungumzia na kila mtu anajua.”

 

Magufuli Alivyoitikisa Mwanza, Ahadi Ya Kuigeuza ’Geveva’
Mahakama Kuu Kuamua Kuhusu Umbali na Kulinda Kura