Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC imemuombea hifadhi nchini Ubelgiji rais wa zamani wa Cote d’Ivoire, Laurent Gbagbo, mara baada ya kuachiwa huru na mahakama hiyo.
Taarifa hiyo imetolewa na shirika la habari la Ubelgiji, Belga. Shirika hilo limemnukuu Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ubelgiji, Karl Lagatie ambaye amesema kuwa nchi hiyo iko tayari kumpokea rais huyo wa zamani kwa sababu ya uhusiano uliopo kati ya nchi hiyo na familia ya Gbagbo.
Aidha, Gbagbo ambaye aliitawala Cote d’Ivoire kuanzia mwaka 2000 hadi 2011, amekuwa jela ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC iliyoko The Hague nchini Uholanzi kwa muda wa miaka saba.
Hata hivyo, Gbagbo na aliyekuwa waziri wake wa masuala ya vijana, Charles Blé Goudé, walifutiwa mashtaka ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu Januari 15, lakini waliendelea kubakia kizuizini wakisubiri pingamizi lililowekwa na waendesha mashtaka ambao wanapanga kukata rufaa kupinga uamuzi wa kuachiwa huru kwa Gbagbo.