Mahakama ya Rufaa imeitaka Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kusikiliza upya kesi ya kupinga matokeo ya Ubunge wa jimbo la Bunda Mjini, iliyofunguliwa na Stephen Wasira (CCM), dhidi ya mbunge wa jimbo hilo, Esther Bulaya (Chadema).

Esther Bulaya

Esther Bulaya

Mahakama hiyo ilikubaliana na hoja ya upande wa mlalamikaji kuwa wapiga kura waliofungua kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kama wakipinga matokeo hayo, wanayo haki ya kufanya hivyo tofauti na ilivyokuwa imeamriwa hapo awali.

Uamuzi huo ulitolewa na jopo la Majaji watano waliosikiliza kesi hiyo wakiongozwa na Jaji Edward Rutakangwa na kusomwa na Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Elizabeth Mkwizu.

Wasira ambaye alikuwa mstari wa mbele kuwasaidia wapiga kura wake kufungua kesi hiyo, amesema kuwa Mahakama ya Rufani imetenda haki na kwamba uamuzi huo utawafaidisha zaidi wapiga kura wake.

Siku moja baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu, mwanasiasa huyo Mkongwe alijitokeza mbele ya waandishi wa habari akipinga matokeo yaliyompa ushindi Esther Bulaya akieleza kuwa baadhi ya fomu za matokeo zilichakachuliwa.

Endapo Mahakama Kuu itaridhika na ushahidi utakaotolewa na wapiga kura waliofungua kesi hiyo, inaweza kumvua ubunge Bulaya na kuitisha uchaguzi mwingine au kuamua vinginevyo inavyofaa.

Hivi karibuni, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilimvua Ubunge, aliyekuwa mbunge wa Longido, Onesmo Ole Nangole (Chadema), na kuamuru uchaguzi urudiwe. Kesi hiyo ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM, Dk Stephen Kiruswa.

Juventus Waipotezea Chelsea, Kufanya Biashara Na Man City
Video: "Tuliahidi kutoa Kero kwa Wananchi..." - Rais Magufuli