Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza makusanyo ya fedha za ndani yatumike katika ujenzi wa miradi ya maendeleo badala ya kutegemea fedha zinazotoka Serikali Kuu. pekee
Majaliwa ameyasema hayo hii leo Julai 11, 2022 baada ya kukutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam na ya wilaya ya Kinondoni.
“Mwaka 2020/2021 mlikusanya zaidi ya shilingi bilioni 40, pamoja na makusanyo hayo makubwa lakini hatuoni mradi mkubwa unaotekelezwa kupitia fedha hizo. Makusanyo ya mapato na matumizi yasimamiwe vizuri na fedha hizo zitumike katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo,” amesema.
Ziara hiyo, yenye lengo la kukutana na viongozi na watumishi wa umma mkoani Dar Es Salaam ili kuwakumbusha wajibu wao na kuwahamasisha kufanya kazi wa bidii, Waziri Mkuu pia amewasisitiza kufanya kazi kwa weledi na uaminifu.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amekagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa kingo za Mto Sinza/Ng’ombe na Mfereji wa Kiboko katika eneo la Mtogole ambapo amewataka wananchi wa maeneo hayo kutunza mazingira na wahakikishe hawamwagi taka ndani ya mfereji huo.
Aidha, Majaliwa ameuagiza uongozi wa Manispaa ya Kinondoni ufanye maboresho ya mradi huo kwa kujenga madaraja madogo madogo yatakayowezesha mtu kutoka upande mmoja wa mto kwenda mwingine, pamoja na kuweka taa katika barabara hiyo.
Waziri Mkuu, pia amekagua maendeleo ya miradi ya ujenzi wa soko la wamachinga katika eneo la Mwenge pamoja na ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu wa Manispaa ya Kinondoni.
Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Innocent Bashungwa amemuhakikishia Waziri Mkuu kuwa watashirikiana na viongozi wa mkoa huo kuhakikisha maelekezo aliyoyatoa yanafanyiwa kazi.
Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Amos Makala amemshukuru Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali ya kutolea huduma za jamii ikiwemo ya afya na elimu.