Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU), Mkoa wa Tabora, Musa Chaulo kuwakamata wote wanaohusika na usimamizi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA), Wilaya ya Uyui kwa tuhuma za ubadhilifu wa fedha za mradi huo.
Majaliwa, ametoa agizo hilo leo Septemba 8, 2022 baada ya kukagua mradi huo, na kuonesha kutoridhika na gharama za ujenzi wa baadhi ya majengo, ikiwemo kibanda cha mlinzi ambacho ujenzi wake umegharimu shilingi milioni 11 na majengo yake kujengwa kwa gharama kubwa tofauti na uhalisia.
Mbali na ujenzi wa kibanda cha mlinzi, pia Waziri Mkuu ameonesha kutoridhishwa na ujenzi wa nyumba za watumishi chuoni hapo ambapo nyumba moja yenye uwezo wa kuchukua familia mbili, inajengwa kwa gharama ya shilingi milioni 114 na tayari wameshatumia zaidi ya shilingi milioni 70 na bado haijakamilika.
Amesema, “Nyumba moja yenye uwezo wa kuchukua familia tatu Wizara ya Afya inajenga kwa shilingi milioni 90 na Ofisi ya Rais (TAMISEMI) wanajenga nyumba za walimu zenye uwezo wa kuchukua familia mbili kwa gharama ya shilingi milioni 57 na wanajenga kwa mfumo wa force account kama mnavyojenga hapa, hii haikubaliki.”
Kutokana na kutoridhishwa na ujenzi wa chuo hicho unaosimamiwa na VETA, Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Burian asimamie ujenzi wa huo ili uweze kukamilika kwa wakati.