Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wahakikishe wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia katiba ya chama ili kuepusha migogoro kwenye maeneo yao.
Amesema kuwa chama chochote ambacho viongozi wake hawazingatii katiba lazima kiwe na migogoro kwani uzingatiaji wa katiba ni miongoni mwa mambo yanayokitofautisha Chama Cha Mapinduzi na vyama vingine vya siasa nchini.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na viongozi wa CCM, wabunge pamoja na baadhi ya viongozi wa mkoa wa Kagera kwenye Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera kilichofanyika mkoani humo.
Aidha, amewasisitiza wanachama na wapenzi wa CCM wasome katiba ya chama na kuzielewa kanuni, taratibu na sera ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo, huku akigawa nakala za katiba ya hiyo kwa viongozi hao na kuwataka wazifikishe hadi kwenye ngazi ya mashina.
Vilevile amesema kuwa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwa nchi nzima unaendelea vizuri na kuhusu changamoto zilizopo katika baadhi ya maeneo nchini wanaendelea kuzirekebisha.
Hata hivyo, ameongeza kuwa lengo lao ni kuhakikisha wanatekeleza ilani kama CCM ilivyoelekeza na ili kujiridhisha kama wanafanya vizuri lazima viongozi wawasimamie watendaji katika maeneo yao na watakapobaini kasoro wasisite kutoa taarifa.
-
Mbunge wa Mafinga akabidhi Magari mawili Idara ya Elimu
-
Tanzania yaalikwa maonyesho ya vipodozi China
-
JPM afanya uteuzi wa Mkurugenzi TEWW