Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakandarasi wa ujenzi wa mradi wa barabara ya mzunguko wa nje wa jiji la Dodoma kuongeza kasi ili mradi huo uweze kukamilika kwa wakati na kwa viwango.
“Kazi inaendela vizuri, tunataka kazi ikamilike ikiwezekana hata kabla ya muda, Rais Samia Suluhu Hassan anatekeleza miradi hii ili iwanufaishe Watanzania, hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha tunasimamia na inakamilika kwa viwango na wakati,” amesema Majaliwa.
Amesema hayo Septemba 04, 2022 alipokagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa barabara ya mzunguko wa nje wa jiji la Dodoma.
Pia, Waziri Mkuu amewataka Wahandisi Wasimamizi wa mradi huo wahakikishe wanasimamia kikamilifu wakandarasi ili barabara hiyo iweze kujengwa kwa viwango vilivyokubaliwa kwenye mkataba wa ujenzi wake.
Akizungumza na watanzania walioajiriwa katika mradi huo, Majaliwa amewataka wawe walinzi wa vifaa vinavyotumika kwenye ujenzi na wahakikishe vifaa vinabaki salama, “Pambaneni na wote wenye nia ya kuiba vifaa hivi, tunataka tupate barabara yenye viwango”
Kaimu Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Salome Kabunda amesema kuwa pamoja na mradi huo kusaidia kupunguza msongamano wa magari jiji la Dodoma pindi utakapokamilika, pia umesaidia kutoa ajira kwa wazawa zaidi ya 800.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu utekelezaji wa mradi huu utawezesha kujengwa kwa vituo vya afya vinne katika mitaa ya Mahomanyika, Veyula, Nala na Ihumwa. Pia yatanunuliwa magari ya wagonjwa manne katika vituo hivyo,” Mhandisi Salome.
Aliongeza kuwa sehemu ya kwanza ya ujenzi wa barabara hiyo kutoka Nala-Veyula-Mtumba hadi bandari kavu ya Ihumwa (Km 52.5) unaojengwa kwa muda wa miezi 39, utagharimu shilingi bilioni 100.
“Sehemu ya pili ya ujenzi wa barabara hii kutoka Bandari kavu ya Ihumwa-Matumbulu hadi Nala (Km 60) unaojengwa kwa muda wa miezi 43, utagharimu shilingi bilioni 120.8,” mhandisi Salome.
Mradi huo ni sehemu ya uendelezaji wa jiji hilo la Dodoma.