Siku ya Wanawake Duniani , ambayo pia inajulikana kama “International Women Day – IWD, inasherehekewa Machi 8, kila mwaka kwa zaidi ya Karne moja sasa, ikitokana na vuguvugu la wafanyakazi linalotambuliwa na Umoja wa Mataifa – UN.
Chimbuko lake ni mwaka 1908, wakati wanawake 15,000 walipoandamana katika Jiji la New York nchini Marekani kudai muda mfupi wa kufanya kazi, malipo bora na haki ya kupiga kura na mwaka mmoja baadaye, Chama cha Kisosholisti cha Marekani kiliitangaza Siku ya Kitaifa ya Wanawake kwa mara ya kwanza.
Wazo la kuifanya siku hiyo kuwa ya kimataifa, lilitoka kwa Mwanaharakati wa kikomunisti, Clara Zetkin, aliyekuwa mtetezi wa haki za Wanawake, ambapo mwaka 1910 alipendekeza wazo kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Wanawake Wafanyakazi Copenhagen, uliokuwa umehudhuriwa na wanawake 100 kutoka nchi 17, na lilikubalika kwa kauli moja.
Kwa mara ya kwanza, iliadhimishwa mwaka 1911, huko Austria, Denmark, Ujerumani na Uswisi na kwa mwaka huu Kitaalam inasherehekewa siku ya 112 ya Kimataifa ya Wanawake na siku ya Kimataifa ikaendelea kufana maeneo mbalimbali, ikiwakutanisha Wanawake pamoja kujadili mafanikio yao katika sekta mbalimbali, changamoto wanazopitia na jinsi ya kuzikabili.
Kauli mbiu ya Siku hiyo kwa mwaka huu (2023), ni “Uvumbuzi na Teknolojia kwa Usawa wa Jinsia,” ikionesha umuhimu wa ujumuishi wao katika masuala ya teknolojia na uvumbuzi, ili kuwawezesha kutimiza ndoto zao katika nyanja mbalimbali.
Ifahamike kuwa, mara nyingi wanawake wamekuwa wakikumbwa na unyanyasaji katika sehemu za kazi, biashara, elimu, na hata ndani ya ndoa na bila shaka huu ni wakati sahihi kwa jamii kuungana ili kuhakikisha haki za mtoto wa kike na wanawake zinatimizwa.
Wanawake wanatakiwa kupewa nafasi sawa na Wanaume katika maeneo ya kazi, muda umefika kuona kuwa, mwanamke si kiumbe dhaifu asiyejiweza, bali kutambua kuwa, mwanamke na mtoto wa kike ni nguvu kubwa katika jamii, na anapopewa nafasi, anaweza kufanya mambo makubwa.
Kwa hapa Tanzania tukio kubwa na ambalo limeweka rekodi katika siku hii kwa upande wa siasa ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi – CCM kuhudhuria mkutano wa wanawake wa chama pinzani cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA.
Hii inaonyesha ni namna gani ambavyo Wanawake wanaweza kuwa kitu kimoja katika kutafuta usawa wa kijinsia kama ambavyo kauli mbiu ya mwaka huu inasema na bila kujali itikadi zao za kisiasa au vyama.
Kauli ya rais samia ya hivi karibu wakati akifunga mkutano wa faragha baada ya kukutana na wateule wake alisema Mkajiamini.
Huku Mkurugenzi wa chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania (Tamwa) Dr Rose ruben akiwataka Wanawake kutumia teknolojia katika kuendesha biashara na kujikuza kiuchumi.
Pamoja na Wanawake kufanya kazi kwa bidii kwa lengo la kujikwamua kiuchumi, pia amewataka kuwa makini na watoto na kuwaepusha na ukatili wa kubakwa na kulawitiwa pindi wanapokuwa mashuleni na hata nyumbani kwa kumpa muda mtoto wa kumsikiliza na kujua nini amepitia kwa siku nzima amabayo mzazi hakuwa naye.
Mitandao ya kijamii kama nafasi mojawapo ya Dunia kijiji inaweza kuwa chachu kwa Wanawake kutumia fursa hiyo kutangaza na kubuni mambo mabalimbali yanayoleta maendeleo ikiwemo biashara na waweze kuitumia sikuu hii muhimu kujipambanua katika nyanja mbalimbali.
Hawa ni wanawake wapambanaji mamalishe ambao ni watu muhimu sana katika maeneo mbalimbali duniani, kina mama hawa hupika chakula na kukiuza kwa watu tofauti tofauti na kujipatia kipato kinachosaidia familia zao.
Mbali na chanagmoto wanazopitia katika kazi hii, wanawake hawa shupavu pia wanamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Saia Suluhu Hassan kwa kuwqtoa juani na kuwaweka kivulini.
Aidha, wamezungumzia pia changamoto ya watoto wao kutokuwepo katika hali ya usalama na kukutwa na ukatili wa kubakwa na kulawitiwa na baadhi ya ndugu, jamaa na hata watu wasiojulikana na wanaiomba Serikali na jamii kwa ujumla kuwalinda watoto pale wao wanapokwenda kusaka tonge.
Kwa mujibu wa tovuti ya Kimataifa ya Siku ya Wanawake, Machi 8 hupambwa na rangi za Zambarau, kijani na nyeupe ambazo ni rangi rasmi za IWD, Zambarau ikiashiria haki na utu huku rangi ya Kijani ikiashiria matumaini na Nyeupe huwakilisha usafi.
Hata hivyo, ikumbukwe kuwa Machi 8 haikuwa siku rasmi iliyopendekezwa wala kurasimishwa bali iliafikiwa kufuatia siku ya mgomo wakati wa vita mwaka 1917, wakati wanawake wa Urusi wakidai “mkate na amani” ambapo siku nne baada ya mgomo huo.
Baadaye, Kiongozi wao alilazimika kujiuzulu na Serikali ya muda iliwapa wanawake haki ya kupiga kura, hivyo tarehe ambapo mgomo wa wanawake ulianza kwa kalenda ya Julian, iliyokuwa ikitumika nchini Urusi, ilikuwa Jumapili Februari 23, sku hii katika kalenda ya Gregori ni tarehe 8 Machi na ndipo iliafikiwa rasmi.
Heri ya siku ya Wanawake Duniani kwa akina mama wote.