Mjadala wa utaratibu uliotumiwa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Dkt. Bashiru Ally kumuita ofisini kwake Bernard Membe limemuibua katibu mkuu wa zamani wa chama hicho, Yusuf Makamba.
Mzee Makamba amemuunga mkono Dkt. Bashiru Ally akieleza kuwa utaratibu wa kumuita mwanachama hadharani haukuanza leo na kwamba hata yeye alikuwa anaitwa kwa njia hizo tangu enzi za TANU.
“Mimi niliwahi kuitwa na [John] Mhavile, nilikuwa Mkuu wa Wilaya ya Tanga. Mhavile alikuwa Katibu Mtendaji wa TANU, yalitokea maneno pale Tanga nikaambiwa njoo, tena sio kwa simu. Niliwahi kuitwa na Mwakawago (Balozi Daudi). Kwahiyo haya mambo sio kwamba ni ya jana,” alisema Makamba.
Alieleza kuwa Mhavile alifika katika uwanja wa Mkwakwani Tanga na wakati anahutubia akamtaja Makamba aliyekuwa mkuu wa wilaya na kutaka afike ofisini kwake lakini hakuna mtu yeyote aliyelalamikia utaratibu huo.
Mtazamo huo wa Mzee Makamba unatofautiana na wa Katibu Mkuu wa zamani wa chama hicho ambaye pia aliwahi kuwa Spika wa Bunge, Pius Msekwa ambaye alikosoa utaratibu uliotumiwa na Dkt. Bashiru akieleza kuwa alipaswa kutumia barua au kumpigia simu Membe.
Aidha, Mzee Makamba katika mifano yake ya kumbukizi, alimtaja pia Msekwa kuwa aliwahi kumuita afike katika ofisi za chama hicho zilizoko Lumumba jijini Dar es Salaam na aliitikia wito huo.
CCM imemtaka Membe kufika katika ofisi ya Katibu Mkuu kujibu tuhuma za kuanza kufanya harakati za kuingilia uchaguzi wa ndani wa chama hicho wa kumpata mgombea urais wa mwaka 2020.