Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) limefanikiwa kukamata makontena tisa katika eneo la Mbezi Tangibovu, Kinondoni, Dar es Salaam.

Akizungumzia sakata hilo, Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipa Kodi TRA, Richard Kayombo alisema kuwa walipata taarifa kutoka kwa wasamilia wema kuwa jana usiku wa manane makontena hayo tisa yalikuwa yakihamishwa kwa siri kutoka katika Bandari kavu ya PMM ambayo iko eneo la Vingunguti jijini humo.

Kayombo alieleza kuwa walishirikiana na Jeshi la polisi kubaini yalipoelekezwa makontena hayo na ndipo walipoyakuta katika eneo la Mbezi Tangibovu. Alisema kuwa makontena hayo yaliwekwa katika ‘godauni’ lililopo eneo hilo, ambalo halitambuliki kisheria.

Mkurugenzi huyo wa Elimu kwa umma TRA, alibainisha kuwa  makontena hayo yanaonekana katika kumbukumbu kuwa yalipata kibali cha kutoka bandarini Septemba 17 mwaka huu lakini kibali hicho hivi sasa kimekwisha muda wake.

“Hiki ni kiashiria kwamba kuna jambo baya lilikuwa linataka kutendeka kama kukwepa kulipa kodi, “Kayombo aliwaambia waandishi wa habari katika eneo la tukio.

Alieleza kuwa tayari Jeshi la Polisi linawashikiria madereva wa magari matatu yaliyosafirisha makontena hayo waliokutwa katika eneo hilo pamoja na magari hayo.

Alimtaka mhusika wa makontena hayo kujisalimisha polisi ndani ya saa 24 kuanzia leo mchana.

Mbunge Afariki Akifanya Mapenzi Kwenye Gari
Zitto Kabwe amng'ang'ania Maalim Seif, Awataka ZEC waepushe Shari