Mbunge wa Mvumi na Mjumbe wa NEC, Livingistone Lusinde, amesema Chama cha Mapinduzi kinaongozwa kwa nidhamu ya hali ya juu na siri, na Mwenyekiti wa chama akisema jambo wanachama wote wanafuata kwa kuwa anakuwa ametoa maelekezo ndiyo maana CCM inakuwa bora hivyo makundi yanayojitokeza yanashughulikiwa mara moja kuhakikisha nidhamu ya CCM inabaki palepale.
Lusinde amesema hayo wakati akizungumza na Dar24 Media Jijini Dodoma katika mahojiano maalum akizungumzia miaka 45 ya CCM na tetesi za kuwa ndani ya Chama kuna makundi ambayo yanagawanyika ili kuanza harakati za kugombea uchaguzi mkuu wa 2025.
”Hayo sio makundi rasmi hayo ni makundi ya waroho, kwa sababu makundi rasmi huwa yanakuja baada ya muda kufika ndiyo maana hata kwenye ubunge na udiwani, uchaguzi ukiisha unasubiri uchaguzi mwingine na utaratibu unatangaza na chama,” amesema Lusinde.
Ameongeza kuwa hata ”baada ya spika kujiuzulu Cham cha Mapinduzi (CCM ) kilitoa ratiba, baada ya spika kuchaguliwa ukatolewa utaratibu kinyume chake inakuwa sio kundi halali inakuwa kundi harama kwahiyo nafikiri hayo ndiyo makundi yanayotakiwa kushughulikiwa”
Lusinde amesema miaka 45 ya CCM imefanya kazi kubwa ya kusimamia Taifa na kuliongoza kwa kuwa na amani na utulivu ambapo amesema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa ya maendelea hata kwa mtu mmoja mmoja toka kipindi cha uhuru mpaka sasa.
”Kwa mara ya kwanza tumempoteza Rais wa Nchi kwa kifo, jambo hilo lingeweza kutupa shida lakini Mheshimiwa Samia Suluhu ameiongoza nchi baada ya tukio kubwa kama hilo na nchi imetulia na kwa mara ya kwanza nchi imepata Rais mwanamke na amefanya mambo makubwa tumejenga madarasa 11,000 kwa mara moja tangu tupate Uhuru,” amesema Lusinde.
Livingstone Lusinde amekuwa katika Halsmashauri Kuu ya CCM kwa vipindi vitano ambapo ni mmoja wa wabunge na wajumbe wa CCM ambao wanaweza kuzungumzia Chama kwa undani kutokana na uwepo wake ndani ya Halmashauri kuu ya CCM kwa muda mrefu.