Kaimu Mkurugenzi-Usimamizi wa Mabenki, Benki Kuu ya Tanzania, (BoT), Eliamringi Mandari amesema kuwa wananchi binafsi wanaweza kukopa mikopo ya fedha za ujenzi, (Mortgage Finance), kwenye mabenki bila ya kuanza kupitia kwenye taasisi nyingine za fedha.
Mandari amesema hayo leo Machi 29, 2017 wakati akiwasilisha mada juu ya utaratibu wa mikopo ya fedha kwa ajili ya ujenzi, na utunzaji taarifa mteja (mkopaji) katika kitunza taarifa cha kibenki, (Databank) kwenye semina ya Waandishi wa Habari za Uchumi na Fedha inayoendelea kwenye ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania tawi la Zanzibar, mjini Unguja.
Amesema watu wengi hawajui kama kuna fursa ya ku-mortgage, kwa maana ya kujenga, kununua au kurekebisha nyumba yako, na katika kudhamiria kufanya hayo, benki inaweza kutoa masharti ambayo ni ya kurejesha mkopo huo kwa muda mrefu kati ya miaka 5 hadi 20.
Aidha, Mandari amesema kama ilivyo kwa masharti mengine yahusuyo kukopa, hata fursa hii ya kukopa fedha kwa ajili ya ujenzi vigezo na masharti pia huzingatiwa ili benki iweze kutoa mkopo huo.
Akizungumza kuhusu mfumo wa taarifa unaosaidia mkopeshaji, (lender), kumjua mkopaji, (borrower), ujulikanao kama, Credit Reference System, (DBS), amesema Sheria namba 48 ya BoT kuhusu masuala ya kubadilishana taarifa za mikopo, kwa mabenki na taasisi nyingine za fedha inalazimisha mabenki na taasisi hizo kutuma taarifa za wateja (wakopaji), kwenye Databank ya BoT kila mwezi.
Amesema kuwa ni kweli Sheria inaitaka Benki Kuu kusimamia taasisi za fedha zinazochukua amana kutoka kwa wananchi, kwa kuwasilisha taarifa hizo za wakopaji kwenye mfumo huo wa BoT wa Databank, lakini kwa sasa wakopaji binafsi na taasisi za hiari zinazojishughulisha na utoaji mikopo ya kifedha, bado sera inaandaliwa ili na wao waweze kusimamiwa.