Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amefanya mazungumzo na Waziri wa Afya wa Marekani, Amiral Brett Giroir kuona namna gani nchi hizo mbili zinaweza kushirikiana katika kupambana na ugonjwa wa Sickle Cell (Seli Mundu) hasa kwa watoto wachanga na wale walio chini ya miaka mitano.
Waziri Ummy amemueleza Waziri huyo kuwa watoto wapatao 11,000 wanazaliwa na ugonjwa huo Tanzania na wengi hupoteza maisha kwa sababu ya kuchelewa kufanyiwa vipimo na kugundulika mapema.
Amesema kuwa muelekeo wa nchi kwasasa ni kuhakikisha kuwa kila mtoto anayezaliwa anapimwa Sickle Cell na watakaogundulika matibabu yaanze mapema ili kupunguza vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.
Aidha, mawaziri hao wamekubaliana kwa pamoja kushirikiana katika kudhibiti vifo vinavyoweza kutokea kwa sababu ya ugonjwa huo huku Waziri, Amiral akiahidi kuimarisha upatikanaji wa vipimo, pamoja na matibabu kwa watoto wanaozaliwa na ugonjwa huo kuanzia ngazi ya zahanati na vituo vyote vya kutoa huduma za afya nchini.
“Ni muhimu huduma hizi zikatolewa katika ngazi ya afya ya msingi mpaka taifa ili kuwapa huduma stahiki wananchi, hii ikiwa ni utekelezaji wa afya kwa wote, Suala la upimaji wa Seli Mundu, elimu kwa jamii na pia suala la matibabu katika ngazi zote za utoaji huduma ni muhimu vikapewa kipaumbele,”amesema Waziri Ummy.
Kwa upande wake Waziri, Brett amepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kwa kujenga viwanda vya dawa nchini ikiwa ni pamoja na za Sickle Cell, pia ameahidi kutembelea Tanzania kuona na kujadiliana zaidi namna nchi hizo mbili zitakavyoshirikiana katika kushughulikia ugonjwa huo nchini.
Mawaziri hao wanahudhuria mkutano wa 69 wa Shirika la Afya Duniani (WHO) unaojumuisha Mawaziri wa Afya toka nchi mbalimbali za Afrika unaoendelea jijini Brazzaville Jamhuri ya Kongo.