Mbunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele ambaye pia ni mbunge wa Bunge la Afrika (PAP), amezungumza na waandishi wa habari baada ya kuhojiwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa tuhuma za utovu wa nidhamu.
Masele ambaye leo alifanikiwa kufika kwa muda mbele ya kamati hiyo akiitikia wito wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai aliyempa ukomo wa muda wa saa tano asubuhi, amesema kuwa anaamini kamati hiyo itamtendea haki.
Ameeleza kuwa hajafanya jambo lolote la utovu wa nidhamu na kwamba alilelewa vizuri ndani ya Chama Cha Mapinduzi tangu ngazi ya chini.
“Nimelelewa vizuri na wazazi, nimelelewa vizuri na chama changu, nimetokea umoja wa vijana kuanzia ngazi ya chini kabisa mpaka ngazi ya kitaifa,” alisema Masele.
Aidha, Masele ambaye pia ni Makamu wa Rais wa PAP ameeleza kuwa anaheshimu viongozi wenzake na kwamba anajua alichokuwa anakifanya katika bunge la PAP na hajawahi kukurupuka.
“Nawahakikishia Watanzania nilichokuwa nakisimamia ni misingi ya haki za binadamu na kufanya hivyo nisitafsiriwe kwamba ni utovu wa nidhamu,” alisema.
Masele aliitwa na Spika Ndugai kurejea nyumbani kwa madai kuwa amekuwa akifanya mambo ya hovyohovyo ikiwa ni pamoja na kuchonganisha mihimili ya Bunge na Serikali.
Wakati Masele anajiandaa kurejea, alikuwa anatarajia kuhudhuria kikao cha uwasilishaji wa ripoti ya kamati maalum aliyoiunda kuchunguza tuhuma za rushwa, ngono na matumizi mabaya ya ofisi dhidi ya Rais wa PAP, Roger Nkodo Dang.