Meneja wa klabu bingwa nchini Italia, Juventus, Massimiliano Allegri, amepangua taarifa za kuhusishwa na mipango ya kutaka kuajiriwa na klabu ya Chelsea itakapofika mwishoni mwa msimu huu.

Allegri, amepangua taarifa hizo kwa kusema bado ataendelea kuwajibika huko Juventus Stadium, kama mkataba wake unavyoeleza, na wala hana mpango wa kuondoka na kusaka mahala pengine pa kufanya shughuli zake za ukufunzi wa soka.

Meneja huyo kutoka nchini Italia, amesema anashangazwa na taarifa ambazo kila leo zimekua zikiandikwa katika baadhi ya vyombo vya habari dhidi yake, ili hali hakuwahi kusema chochote kuhusu mustakabali wa maisha yake baada ya kuondoka Juventus ama mwishoni mwa msimu huu utakapofika.

Amedai kwamba kuna, baadhi ya watu walikua wanahitaji kusikia ni nini atakachokizungumza baada ya kuzushwa kwa taarifa hizo, na anaamini kwa sasa wamepata uhakika kwamba ataendelea kubaki Juventus Stadium.

Hata hivyo Allegri ambaye aliwahi kukinoa kikosi cha AC Milan amesisitiza kwamba kuandikwa kuhusu kuondoka Juventus na kuhusishwa na mipango ya kujiunga na klabu nyingine kubwa barani Ulaya kama Chelsea, ni hatua kubwa sana kwake na inaonyesha ni vipi anavyofanya kazi zake za kila siku kwa uhakika ambao unafuatiliwa na kila mmoja.

Allegri, alikabidhiwa jukumu la kukiongoza kikosi cha Juventus, mwaka 2014 baada ya kuondoka kwa Antonio Conte aliyetangaza kujiuzulu nafasi yake na kisha kuajiriwa na chama cha soka nchini Italia kama kocha wa timu ya taifa ya nchi hiyo.

Mpaka sasa Allegri ameshaiwezesha Juventus kutwaa ubingwa wa nchini Italia (Scudetto) mara moja msimu wa 2014-15, kombe la Italia (Coppa Italia) mara moja mwaka 2015.

Mafanikio mengine ni kumaliza kama mshindi wa pili wa michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu uliopita baada ya kufungwa na FC Barcelona pamoja na kushindwa katika mchezo wa ufunguzi wa ligi ya nchini Italia msimu wa 2014-15 (Supercoppa Italiana) kwa kukubali kufungwa na Napoli mabao mawili kwa sifuri, huku akirekebisha makosa yake kwa kutwaa ubingwa huo mwanzoni mwa msimu huu, kwa kuifunga Lazio mabao mawili kwa sifuri.

Mata Awaomba Radhi Mashabiki Wake
Dubai Ni Mahala Sahihi Kwa Rooney Kujifariji