Golikipa mahiri wa Mbeya City, Haningtony Kalyesubula amesema kupatikana kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya African Sports ya Tanga kwenye mchezo wa ligi kuu ya soka Tanzania Bara uliochezwa jana kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya limekuwa ni jambo zuri lililokuwa likihitajiwa na kila mmoja.

Akizungumza mapema leo na Kalyesubula ambaye alikosa michezo kadhaa ya mwanzo wa msimu kutokana na maumivu ya kidole gumba alisema kuwa City imekuwa nje ya ushindi kwa takribani michezo zaidi ya 7 hivyo kila mmoja kikosini alikuwa na hamu ya kupata pointi tatu.

“Tuliingia uwanjani kucheza na Sports lengo letu likiwa moja tu, kushinda, kila mmoja alikuwa na shauku na poiti tatu ambazo tulizikosa kwenye michezo 6 au 7 ya mwanzo, tulikuwa bora sana kwa sababu tuliamua kupambana, nashukuru mungu kuwa lengo la kila mmoja lilitimia baada ya dakika 90” alisema.

Akiendelea zaidi golikipa huyo ambaye alifanikiwa kucheza michezo 9 ya mzunguko wa pili wa ligi ya Vodacom msimu uliopita akichukua nafasi ya David Buruhan aliyetupiwa viwango na kufungwa mabao 8 pekee aliweka wazi kuwa ilikuwa ni vigumu kushinda mbele ya Sports ambayo pia ilitoka kupoteza mchezo huko Songea lakini mbinu za mwalimu Mingane zilisaidia kuifunga timu hiyo kutoka Tanga.

“Ulikuwa mchezo mgumu, Sports walipoteza mchezo uliopita huko Songea walikuja wakitaka kujiweka sawa, nadhani mbinu bora za mwalimu zilitusaidia, tulishambulia kwa kasi sana kwa sababu tuna wachezaji wenye kasi, sikatai wapinzani wetu walicheza vizuri pia hasa kipindi cha pili lakini matokeo baada ya dakika 90 yalidhihirisha sisi tulikuwa bora kuliko wao, hakika ilikuwa siku nzuri sana kwetu wachezaji,wadau na mashabiki wetu” alimaliza.

Magufuli Ajisogeza Zaidi Kwa Wafanyakazi
Kocha Wa Taifa Stars Kurejea Afrika Mashariki