Serikali imewataka Watanzania kutembea kifua mbele na kujivunia mbegu mpya ya mchikichi ambayo imeonesha mafanikio makubwa baada ya kufanyiwa utafiti.
Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akihitimisha kikao chake na wadau wa zao la chikichi Mkoani Kigoma na kuzungumzia namna mbegu hiyo bora ya michikichi aina ya TENERA inavyotoa mafuta mara tatu zaidi ya aina ya DURA ambayo inalimwa na wakulima kwa asilimia 90.
Amesema, ” leo nimesikia michango ya wadau wote. Nimejiridhisha kwamba utafiti tulioufanya wa kuzalisha mbegu ya Tanzania ambayo inaota na kutoa matunda ndani ya miaka miwili hadi mitatu umefanikiwa.”
Kufuatia ufanisi huo, Waziri Mkuu amezitaka Halmashauri zinazolima zao la chikichi, ziimarishe vitalu vya miche ya zao hilo na kufanya ufuatiliaji wa karibu kwa ile inayopelekwa kwa wakulima, ili ikue na kufikia hatua ya kuzaa.