Mchakato wa Uchaguzi Mkuu nchini umekuwa wa kipekee na wenye matukio ambayo watanzania hawakuwahi kuyashuhudia huku wengi wakibaki njia panda wasijue kinachofanyika na filamu au uhalisia.

Kufuatia tukio la kihistoria la waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa kujiunga rasmi na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo kilichokuwa kikimtuhumu mara kwa mara kuwa fisadi, mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe aliweka wazi kuwa waliudanganya umma mara kadhaa ili kukichanganya Chama Cha Mapinduzi.

Akitoa ufafanuzi baada ya kumpokea rasmi na kumkabidhi kadi ya uanachama Edward Lowassa, Mbowe alisema kuwa makada wa Chama Cha Mapinduzi walimpigia simu mara kwa mara mwenyekiti huyo wakimtahadharisha kutompokea Lowassa kwenye chama hicho kwa madai kuwa atakiharibu.

Kwa mujibu wa Mbowe, aliamua kuwadanganya kwa msisitizo kuwa hawezi hata siku moja kumkaribisha Lowassa na kwamba hicho ni kitu kisichowezekana zaidi katika dunia hii, “niliwaambia kama kuna kitu kisichowezekana duniani, ni hicho. Tena nikatumia kiingereza, ‘over my dead body’.”

Alieleza kuwa hata alipofuatwa na vyombo vya habari alilazimika kusema kuwa Lowassa ni dhaifu na hawezi kujiunga na Chadema. Bila shaka alisema hivyo akijua dhahiri kuwa ujumbe huo utaufikia umma lakini sio ujumbe halisi.

Hata hivyo, dhamira yake ilikuwa kuichanganya CCM isijue mpango wake kwa kuwa alijua wanahofia uamuzi atakaouchukua. “Nilifikiria…tangu lini CCM ikaitakia mema Chadema!” Alisema Mbowe.

Udanganyifu huo wenye lengo la kuichanganya CCM umeonekana pia kupitia kauli za hivi karibuni za Edward Lowassa baada ya kuwepo tetesi nyingi kuwa amepanga kukihama chama hicho.

“Mimi ni mwanachama wa CCM tangu mwaka 1977. Nimekuwa  mwanachama wa CCM sijawahi kufanya kazi na chama tofauti zaidi ya Chama Cha Mapinduzi. My life ni CCM, huyu mbaya asiyenitaka CCM yeye ndiye ahame,” alikaririwa Edward Lowassa.

Hata hivyo, yote hayo yameonekana kama maelezo yaliyotolewa kwa makusudi huku vikao mbalimbali kati ya Chadema na timu ya Lowassa vikiendelea kwa usiri mkubwa kabla ya kuonekana picha katika mitandao.

Hata baada ya kuonekana picha hizo, gazeti la Tanzania Daima linalomilikiwa na Mbowe lilimkariri mwenyekiti huyo wa Chadema akizikana picha hizo na kudai kuwa ni za kutengenezwa. Kumbe zote zilikuwa harakati za kudanganya kwa makusudi.

mbowe na

Jana, Mbowe aliweka wazi kuwa alifanya udanganyifu huo makusudi na kuuita ‘mkakati wa ‘over my dead body’ na kwamba ilikuwa mbinu ya kubadili gia hewani.

Alieleza kuwa Chadema wamefanya uamuzi huo baada ya kutafakari na kugundua kuwa una faida zaidi kwa umma na chama hicho na kwamba umefanyika baada ya kusikiliza vizuri maelezo ya Lowassa na kumuelewa.

“wapo watu wengi ambao huko nyuma tuliwatukana sana lakini leo tunawapokea,” alisema Mbowe na kuongeza kuwa hawezi kuacha kupokea watu zaidi ya milioni wanaingia kwenye chama hicho kwa sababu zisizo na msingi kwa sasa.

Ukawa wanategemea kumtangaza mgombea wa urais mapema Agosti 4 mwaka huu huku wengi wakitarajia kuwa atakuwa mwanachama mpya wa Chadema, Edward Lowassa.

Mwinyi Kazimito Ahofia Kucheza Soka Misri
TAKUKURU Yamhoji Mwigulu Nchemba Tuhuma Za Rushwa