Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ameweka wazi hali ya vyama vya siasa vinavyounda Ukawa, kuhusu ‘saintofahamu’ inayojitokeza na kukwamisha uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, na marudio ya uchaguzi wa Zanzibar.

Akiongea na waandishi wa habari baada ya kuhudhuria misa ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la KKKT Wilayani Hai, Mbowe ambaye ni mwenyekiti mwenza wa Ukawa, amesema kuwa umoja huo umechoshwa na kile alichokiita uonevu wa dhahiri unaofanywa na CCM kwa kutumia vyombo vya dola kuzima haki ya vyama hivyo na uamuzi wa wananchi.

“Uvumilivu una mwisho. Uchaguzi tulimaliza mwaka jana, Watanzania walichagua viongozi wao wanaowataka lakini tunaona bado CCM inatumia nguvu au inategemea sana nguvu ya dola katika kumaliza tatizo la Zanzibar,” alisema.

“Hali kadhalika, kwa hali ya jiji la Dar es Salaam, ni miezi minne leo hajapatikana Meya wa jiji la Dar es Salaam kwa sababu ambazo kwakweli hazina msingi wala mashiko yoyote,” aliongeza.

Alieleza kuwa CCM wanazungusha uchaguzi wa Meya wa jiji la Dar es Salaam baada ya kubaini kuwa hakuna namna wanayoweza kushinda kutokana na wingi wa madiwani wa Ukawa, huku wakitaka kuhakikisha wanashinda nafasi hiyo.

“Mimi nachojaribu kusema kwa viongozi wetu hawa wa Serikali watambue kwamba uvumilivu una mwisho. Na tumechoka kuitwa kwenye vikao vya kuchagua Mameya ambao hawachaguliwi. Tumechoka kuona uwakilishi wa wananchi wetu unaingia dosari kwa sababu tu watawala wanataka tu anaongoza atoke kwenye chama chao,” alisisitiza Mbunge huyo wa Hai.

Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam aliahirisha uchaguzi wa Meya wa Jiji hilo kwa sababu CCM walikuwa wamewasilisha pingamizi mahakamani.

 

 

Kiongozi wa Uporaji Benki aonja joto la Magufuli
Walimu kuanza kupanda daladala Bure