Baada ya kushuka daraja, Kocha Mkuu wa Ruvu Shooting, Mbwana Makata, amesema kuna ‘mlolongo’ wa sababu mbalimbali zilizopelekea timu hiyo kushindwa kufanya vizuri katika Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo inakaribia ukingoni.

Mei 12, mwaka huu, Ruvu Shooting ilishuka daraja rasmi ilipokubali kuchapwa mabao 3-0 dhidi ya Simba, mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam na kuifanya kusalia na pointi zake 20.

Kipigo hicho kiliisafirisha timu hiyo kutoka Ligi Kuu na kwenda Championship kwa sababu hata ikishinda mechi mbili zilizobaki itafikisha pointi 26 tu ambazo itakuwa imeipita timu moja tu ya Polisi Tanzania.

Makata amesema usajili wa wachezaji wasiokuwa na viwango vinavyoitakiwa kwa sasa ni sababu kuu iliyowafanya washindwe kuendana na ushindani uliopo.

“Vitu vingi vimesababisha timu ishuke daraja, ikiwamo usajili wa mwanzo wa msimu. Tulikosea kwenye kusajili, wakasajiliwa wachezaji ambao uwezo wao sio ule mkubwa wa kucheza Ligi Kuu. Siku hizi ligi imekuwa nguvu sana Tanzania, unatakiwa uwe na wachezaji wenye uwezo mkubwa, hata wachache ili kukabiliana na timu nyingine.

“Timu nyingi kwa sasa zinasajili wachezaji wa hali ya juu. Uliona kwenye mechi dhidi ya Simba, mipango yote ilikuwa sahihi, lakini tulichozidiwa ni kiwango cha mchezaji mmoja mmoja,” alisema Makata.

Ameongeza hata kipindi cha dirisha dogo hakukuwa na fungu la usajili, badala yake walisajili mchezaji mmoja (Valentino Mashaka), tu hivyo ilikuwa ngumu kukabiliana na baadhi ya timu ambazo zimesajili na kuwekeza kwenye wachezaji bora.

Arsenal yajipeleka kundi la kifo UEFA 2023/24
Wakurugenzi CPB wapigwa msasa mafunzo utawala bora