Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa ametoa hundi za mamilioni ya fedha kwa wadau waliokidhi vigezo vya kukopa kwenye mfuko wa Utamaduni na Sanaa huku akiwataka wasanii na wadau kuomba kukopeshwa fedha za mfuko huo uliofufuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuwakwamua kiuchumi.
Tukio hilo, limefanyika Desemba 23, 2022 jijini Dar es Salaam akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi kwenye uzinduzi rasmi wa utoaji mikopo ulihudhuriwa na viongozi na wadau mbalimbali wa sekta ya Sanaa na Utamaduni.
Aidha, katika uzinduzi huo wadau wa tano kati ya kumi na tisa waliowasilisha maombi yao walipatiwa mikopo yao na Waziri Mchengerwa amefafanua kuwa dhamira ya Serikali ni kuona kuwa kila Mwananchi (msanii au mdau wa sanaa), mwenye sifa ya kukopa aweze kupata fedha ya kuboresha kazi zake.
Amesema, “Naomba nieleweke vizuri fedha hizi ni za kila mtanzania, kila mwana sanaa, kila Kijiji, kila kata, kila wilaya, kila mkoa, yule ambaye anaamini ana kazi yake ameitengeneza, yule ambaye anaamini ameandaa muswada wake vizuri, awe Tanga awe Dodoma awe songea, awe Mtwara atazipata ikiwa tu ana sifa.”
Hata hivyo, amelielekeza Baraza la Sanaa nchini kuandaa utaratibu wa kutengeneza mfumo ya kimtandao ambao utawafanya waombaji kutoka sehemu mbalimbali nchini kuweza kuomba wakiwa huko huko na kupatiwa huduma badala ya kusumbuka kuja Dar es Salaam.
Awali akiongea mahala hapo, Waziri Mchengerwa aliwataka watendaji kujiongeza kwa kushirikiana na wadau ili kupata fedha zaidi za kuwasaidia wasanii ili waweze kuwakopesha viwango vikubwa ambavyo vitakidhi matakwa ya waombaji hao huku Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hassan Abbasi akimtambulisha Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Utamaduni Sanaa, Bi. Nyakaho Mturi Mahemba.