Wakati Young Africans ikiwa kwenye mgogoro wa Kimkataba na Mdhamini Mkuu wa Klabu hiyo SpotPesa, Klabu ya Simba SC imetangaza wazi kuwa, Juma lijalo itamuweka hadharani mdhamini watakaeenda naye kwenye Michuano ya Kimataifa msimu huu 2022/23.

Simba SC kwa misimu miwili mfululizo ikicheza Hatua ya Robo Fainali Barani Afrika, imekua ikivaa jezi zenye udhamini wa ‘Visit Tanzania’, kufuatia kanuni za Michuano ya Kimataifa kuzibana Klabu Shiriki kudhaminiwa na Kampuni za ubashiri.

Mwenyekiti wa Simba SC Murtaza Mangungu amesema wanatarajia kumuanika hadharani Mdhamini watakaeenda naye kwenye Michuano ya Kimataifa, baada ya kuzungumza na Mdhamini mkuu wa Klabu klabu hiyo M-Bet ambaye haruhusiwi Kimataifa kuanzia Hatua ya Makundi.

Amesema Maamuzi ya mazungumzo waliofanya na M-Bet yameshawasilisha CAF kwa kupata ufafanuzi, na wanatarajia hadi juma lijalo watakuwa na jibu sahihi, na ndipo mdhamini mpya atakayetumika kwenye michuano ya Kimataifa atatangazwa hadharani.

“Tumefanya majadiliano na wadhamini wetu (M-bet) na tumepeleka (CAF) na wiki ijayo tutatangaza Mdhamini wa michuano hiyo ya (CAF atakayekaa kifuani), tambua kuwa Simba ndio baba wa matukio” amesema Murtaza Mangungu

Simba SC itaanza kupambana dhidi ya Horoya AC katika mchezo wa Kundi B, lenye timu nyingine za Raja Casablanca (Morocco) na Vipers SC (Uganda).

Simba SC itacheza dhidi ya Horoya AC mjini Conakry, katika Uwanja wa General Lansana Conté, Februari 11 majira ya saa kumi jioni kwa saa za Guinea, huku Raja Casablanca (Morocco) ikiikaribisha Vipers SC (Uganda) Stade Mohammed V, mjini Casablanca, saa mbili usiku kwa saa za Morocco.

Wapinzani wa Young African wamesajili tena
KMC FC yaifuata Ruvu Shooting Morogoro