Jeshi la Polisi nchini linamshikilia Meneja wa benki ya CRDB tawi la Chanika jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kuhusika katika tukio la unyangányi wa kutumia silaha za moto.

Kamanda wa Jeshi la Polisi kanda maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova amewaambia waandishi wa habari jana kuwa jeshi hilo linamshikilia meneja huyo pamoja na watu wengine watatu ambao wanaaminika kula njama na kuvamia benki na kupora, tukio lililosababisha vifo vya walinzi wawili wa suma JKT.

Kwa mujibu wa Kamanda Kova, kabla ya tukio hilo, kamera za CCTV katika benki hiyo zilizimwa kwa muda wa saa 24 hali iliyoashiria kuwa wafanyakazi wa benki hiyo walihusika kula njama katika tukio hilo.

Alisema jeshi hilo lilipomhoji meneja huyo kuhusu kuzimwa kwa kamera za CCTV hakuwa na majibu.

“Kama mnakumbuka tukio la wizi kama hili liliwahi kufanyika katika benki ya Backlays, meneja alifanya vikao na wezi na kuwaeleza kwamba wakifika wampige kibao kimoja, hivyo na huyu meneja wa CRDB Chanika atakuwa kacheza mchezo ule,” alisema Kamanda Kova.

Kamanda Kova alieleza kuwa tukio hilo lilifanyika Disemba 8 ambapo wezi hao walifanikiwa kupora shilingi milioni 20. Aliongeza kuwa polisi wamebaini kuwa watuhumiwa hao pia huwa wanajihusisha na vitendo vya kigaidi.

Rais Magufuli Aapisha Baraza La Mawaziri
Azam FC Huenda Wakafunga Safari Ya Afrika Kusini 2016