Mlinda Mlango wa Young Africans Metacha Mnata ameomba radhi kufuatia zogo lililoibuka baada ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting uliochezwa jana Alhamis, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Metacha alionesha hasira dhidi ya mashabiki na wanachama wa Young Africans, ambao walimlaumu hadharani kwa kumini alionesha kiwango kibovu katika mchezo huo, hasa baada ya kukubali kufungwa bao la pili.

Metacha ambaye amesimamishwa kwa muda na Uongozi wa Young Africans kufuatia sakata hilo, ametumia muda wake leo mchana na kuomba radhi kwa kitendo kilichojitokeza baada ya mchezo dhidi ya Ruvu Shooting.

Kwa mujibu wa Ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram Metacha ameandika : “Kwa niaba ya familia yangu, Management yangu na mimi mwenyewe napenda kuchukua fursa kuomba msamaha kwa Viongozi wa Klabu yangu ya Yanga SC, Wachezaji wenzangu, Benchi la Ufundi na Washabiki wa Klabu ya Yanga, Mamlaka za soka nchini na wadau wote wa soka ambao wamekwazika kwa kwa kitendo nilichokifanya jana.

“Nikiri hakikuwa kitendo cha kiungwana, hivyo najutia makosa niliyoyafanya. Mimi kama mchezaji wa Yanga na Timu ya Taifa napaswa kuwa mfano mzuri siku zote mbele za watoto wanaotamani kuwa kama mimi ambao aidha walikuwepo kiwanjani au waliona mechi kupitia Televisheni majumbani kwao.

“Natambua mchango na umuhimu wa mashabiki kwangu binafsi na kwa Klabu, hivyo kitendo kile hakikupaswa kutokea.

Natanguliza Shukrani.

Video: Harmonize afunguka ya Kajala
Dkt. Gwajima: Makatibu wa Afya hili ni jukumu lenu