Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita anatarajia kuhudhuria mkutano wa Majiji utakaofanyika katika Mji wa Bashar Nchini Iran, ambapo mara baada ya mkutano huo atapata fursa ya kukutana na Rais wa nchi hiyo, Hassan  Rouhani kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Meya wa Jiji la Dar es salaam, imesema kuwa baada ya mkutano huo ataelekea katika Jiji la Tehran kwa mwaliko wa Meya ya Jiji hilo.ambapo watajadiliana masuala ya mahusiano ya kibiashara kati ya majiji hayo mawili.

“ Iran na Tanzania ni nchi marafiki kwa kipindi kirefu kwa hiyo utaona kwamba mambo mengi wamekuwa wakishirikiana na sisi, ni fursa pia kwa majiji haya mawili kubadilishana uwezo wa kuendeleza jiji letu, “ amesema Mwita.

Aidha, ameongeza kuwa akiwa nchini humo atapata fursa ya kushuhudia kampeni za uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo ambapo miongoni mwa wagombea wa nafasi ya urais ni Meya wa Jiji la Teheran.

Hata hivyo, Meya ametoa wito kwa wakazi wa Jiji la Dar es salaam wanaoishi mabondeni kuchukua tahadhari kwani bado mvua zinaendelea kunyesha hivyo wajikinge na mafuriko.

Video: CUF wakiri vijana wao kufanya vurugu kwenye mkutano
Arsene Wenger Aeleza Kinachomuweka Benchi Iwobi