Askari wa Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani, wametakiwa kutumia kikamilifu Mfumo wa Kielektroniki – RAMIS, kubaini makosa ya usalama barabarani pamoja na ukusanyaji madeni.
Agizo hilo, limetolewa na Mkuu wa Oparesheni na Mafunzo Tanzania Kamishna wa Polisi, Awadhi Jumanne Mkoani Singida akiwa katika ziara ya kikazi.
CP Awadhi pia amewahimiza watendaji wa kikosi hicho wakiwemo Wakuu wa Usalama Barabarani wa Mikoa na Wilaya zote nchini, kuhakikisha wanasimamia vyema suala la usalama barabarani ili kudhibiti ajali hasa katika kipindi hiki cha msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.
Aidha, amewaelekeza kutokumfumbia macho dereva yeyote atakayevunja sheria za usalama barabarani kwa makusudi ikiwemo kuendesha kwa mwendokasi au kulipita gari lingine sehemu ambazo haziruhusiwi au kutenda vitendo vyovyote vya uvunjifu wa sheria za usalama barabarani ambazo zinaweza kuhatarisha maisha ya watu.