Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendelo ya Kilimo – TADB, inatekeleza mradi wa kutoa mikopo yenye masharti nafuu na isiyo na riba ya pembejeo za ufugaji samaki ikijumuisha vizimba, vifaranga vya samaki na chakula cha samaki kwa ajili ya ufugaji samaki kwa njia ya vizimba.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, David Silinde ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Busanda, Mhe. Bryceson Magessa Tumaini kuhusu mkakati wa Serikali katika kuwawezesha wavuvi ambao wameunda vikundi na kuanza ufugaji wa vizimba katika Jimbo la Busanda.
Amesema, jumla ya wavuvi 3,154 wameainishwa kunufaika na mradi huo ikijumuishwa vikundi 93, kampuni 10, na watu binafsi 32. Aidha, kwa upande wa Halmashauri ya Geita, vikundi vitatu vinatarajiwa kunufaika na program hiyo ikiwemo kikundi cha Tumaini chenye wanachama 10 kutoka Jimbo la Busanda.
Silinde ameongeza kuwa, vikundi hivyo vitapatiwa mikopo ya pembejeo za ufugaji samaki kwenye vizimba yenye thamani ya shilingi milioni 69.4 kwa kila kikundi. Pembejeo zinazotolewa ni pamoja na vizimba, vifaranga vya samaki na chakula cha samaki.
“Katika mwaka 2023/2024, Serikali itaendelea kutekeleza mradi wa kutoa mikopo yenye masharti nafuu na isiyo na riba ya pembejeo za ufugaji samaki kwa kuwezesha ufugaji samaki kwenye vizimba 893. Hivyo, natoa wito kwa wafugaji samaki nchini wakiwemo wale wa Jimbo la Busanda kuendelea kuchangamkia fursa hii kwa kujiunga katika vikundi na kuanzisha vyama vya ushirika wa ufugaji samaki,” alisema Silinde.