Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewaagiza Mkuu wa Mkoa wa Mtwara pamoja Mkuu wa Wilaya kukaa pamoja na wananchi wa Kijiji cha Msimbati, ili mpango wa maendeleo wa kijiji hicho uandaliwe na fedha zinapotolewa zifanye maendeleo kulingana na mpango wa kijiji.
Dkt. Biteko ametoa maagizo hayo wakati aliposimama katika Kijiji cha Msimbati wilayani Mtwara, Mkoa wa Mtwara ili kuzungumza na wananchi akiwa anatokea kukagua visima vya kuzalisha na mitambo ya kuchakata Gesi ya Mnazi Bay iliyopo katika Kata ya Msimbati wilayani humo.
Aidha, pia ameiagiza TPDC kuweka mpango maalum wa Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo kwa Jamii (CSR) katika eneo hilo ili wananchi hao waone faida ya kuwepo kwa miradi kwenye maeneo yao na kuwaelekeza kuwaagiza wajenge kituo cha afya, taa za barabarani na Kituo cha Polisi.
Ili kuhakikisha kuwa jamii zinazozunguka na miradi ya Mafuta na Gesi Asilia zinafaidika na uwepo wa miradi hiyo, Dkt. Biteko amesema Serikali itakuja na kanuni zitakazoongoza masuala ya CSR lengo likiwa ni kuhakikisha jamii zinazozunguka miradi ya Mafuta na Gesi zinanufaika.