Serikali Mkoani Dodoma imeendelea kuimarisha miundombinu katika sekta ya Elimu na Afya kwa lengo la kuboresha na kusogeza huduma kwa wananchi huku ikiwaasa watumishi kuwa na weledi, ushirikiano, kupendana na kuepuka kufanya kazi kwa mazoea.
Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Ally Gugu ameyasema hayo wakati alipofanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Chemba kukagua miradi ya maendeleo na kudai kuwa ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa madarasa, maabara na zahanati katika Vijiji vya Jangalo, Soya na Ombiri.
Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Ally Gugu akikagua jengo la utawala ikiwa ni sehemu ya ujenzi wa Zahanati ya Mlongia, Wilaya ya Chemba. Zahanati ya Mlongia iko katika hatua za mwisho za ukamilishaji na kiasi cha Shilingi milioni 50 zimetolewa na Serikali katika kukamilisha ujenzi wake.
Amesema, “ndugu zangu Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya kukamilisha miradi hii ya maendeleo, nitoe rai kwenu kwanza kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati, pili miradi ikamilike kwa ubora wa hali ya juu.”
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, Siwema Jumaa amesema mbali ya fedha kutoka Serikali kuu utekelezaji wa miradi hiyo ni pamoja na jitihada za nguvu za wananchi ambao kwa baadhi ya majengo ya zahanati na madarasa wananchi wamejenga maboma.