Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeingia mkataba wa mashirikiano na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, katika matumizi na ujenzi wa miundombinu ya mkongo wa Taifa kwa kutumia miundombinu ya umeme.
Makubaliano hayo yamesainiwa na Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka na Katibu Mkuu Wizara ya Teknolojia na Mawasiliano ya Habari, Dkt. Zainabu Chaula, yakishuhudiwa na Mawaziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani na Waziri wa Teknolojia na Mawasiliano ya Habari Dkt. Faustine Andungulile.
Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, Mwinuka amesema lengo la kushirikiana ni kuwepo kwa matumizi mazuri ya fedha katika uwekezaji wa miundombinu hiyo.
“Ushirikiano huu utatusaidia kuwafikia wananchi kirahisi zaidi, kuliko kila Taasisi kufanya kwa peke yake, lakini vile vile tutapata dhamani ya fedha ambayo Serikali inaitoa” amesema Dkt Mwinuka.
Ameongeza tukio la makubaliano ni muhimu kwa pande zote mbili kutokana na kuwa itamsaidia Mhe. Rais kutimiza azma ya kufikisha umeme na mawasiliano kwa kila mwananchi.
Kwa upande wake Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema kusainiwa kwa makubaliano hayo kati ya TANESCO na Wizara ya Mawasiano na Teknolojia ya Habari, pande zote mbili zimepata majukumu ya kufanya.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile amewapongeza wataalamu kwa kufanikisha kuanza kwa ushirikiano kati ya Taasisi zilizo chini ya Wizara hizo.