Mahakama ya Kijeshi nchini Sudan Kusini imeanza kusikiliza kesi ya uhaini dhidi ya aliyekuwa mkuu wa majeshi ya nchi hiyo, Jenerali Stephen Buoy Rolnyang.
Jenerali Rolnyang anatuhumiwa kupanga njama ya kuasi dhidi ya Serikali ya Rais Salva Kiir Mayardit na kuwashawishi wanajeshi kumuunga mkono.
Msemaji Msaidizi wa Jeshi la Sudan Kusini, Santo Domic Chol amekaririwa na Aljazeera akisema, “Jenerali Rolnyang anashtakiwa kwa uhaini, kutotii mamlaka ya juu yake pamoja na kutishia usalama wa taifa.”
Domic Chol amefafanua kuwa Jenerali huyo alikamatwa Mei 2018 mwaka jana katika eneo la Mayom, baada ya kukataa kujisalimisha kwenye makao makuu ya jeshi mjini Juba kama alivyotakiwa na Serikali.
Hii sio mara ya kwanza kwa nchi hiyo kuwashtaki maafisa waandamizi wa jeshi na wanasiasa kwa makosa ya uhaini.
Mwaka 2014, Mahakama ya Juba ilisikiliza kesi dhidi ya majenerali wawili wa jeshi kwa tuhuma za kupanga jaribio la mapinduzi. Hata hivyo, waliachiwa baadaye bila kutumikia vifungo vyao kutokana na makubaliano ya amani yaliyoingiwa mwaka 2018.
Sudan Kusini iliingia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2013, baada ya Rais Salva Kiir kumtuhumu aliyekuwa Makamu wake, Riek Machar kwa kupanga njama za kumpindua.
Vita hivyo vilisababisha vifo vya watu zaidi ya 380,000 na watu takribani milioni nne wakimbia nchi hiyo kukwepa vita.