Kocha Mkuu wa timu ya Taifa Tanzania ‘Taifa Stars’ inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Charles Boniface Mkwasa amesema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo wa kesho dhidi ya Algeria kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Urusi.

Akiongea katika mkutano na waandishi wa habari leo, Mkwasa amesema wamejiandaa kuhakikisha wanafanya vizuri katika mchezo huo, wanajua Algeria ni miongoni mwa timu bora Afrika, lakini hilo halitawazuia kuibuka na ushindi.

“Katika mpira wa sasa duniani hakuna timu kubwa wala timu ndogo, lolote linaweza kutokea, sisi tuna nafasi ya kufanya vizuri tukiwa katika uwanja wa nyumbani na washabiki wetu” alisema Mkwasa.

Aidha Mkwasa alisema wamefanya mazoezi kwa pamoja kwa takribani siku 10, vijana wapo katika hali nzuri, hakuna majeruhi vijana wote wapo katia hali nzuri na timu imefanya mazoezi ya mwisho leo asubuhi kabla ya kushuka dimbani kuwakabili Mbweha wa Jangwani.

Mwisho Mkwasa amewaomba watanzania kujitokeza kwa wingi uwanja wa Taifa kuja kuwapa sapoti vijana watakapokuwa wanapeperusha bendera ya Tanzania.

Mechi kati ya Tanzania dhidi ya Algeria kesho Jumamosi itaanza saa 10:30 jioni katika uwanja wa Taifa jijini Dares salaam.

Mwambusi Na Tiketi Ya Kinnah Phiri MCCFC
Filamu Mpya Ya James Bond Yampeleka Tena Kileleni