Viungo wapya waliosajiliwa na timu ya Simba toka Mtibwa Sugar, Mohammed Ibrahim na Muzamir Yasin wameapa kurejesha heshima ndani ya klabu hiyo iliyopotea kwa miaka kadhaa.

Simba ambayo inakisuka kikosi chake ili kufanya vizuri msimu ujao inaamini viungo hao wanaweza wakaleta mabadiliko makubwa ya kiuchezaji ambayo yatarejesha heshima iliyopotea.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viungo hao wameonyesha wanafahamu kuwa mashabiki wa klabu hiyo wanataka mafanikio na kwamba wao kwa kushirikiana na wachezaji waliowakuta watahakikisha wanaisaidia klabu hiyo kuchukua ubingwa msimu ujao.

“Simba ni timu kubwa ina mashabiki wengi ambao wamekosa furaha kwa muda mrefu ni wajibu wangu kushirikiana na wenzangu kuwapa raha mashabiki na wapenzi wake,” alisema Muzamir ambaye alikuwa kiungo wa kutumainiwa wa Mtibwa.

Kwa upande wake Ibrahim alikiri kuwa Simba ina viungo wazuri kama Justice Majabvi, Jonas Mkude,Saidi Ndemla, Mwinyi Kazimoto na wengineo lakini atahakikisha anajituma zaidi na kufuata maelekezo ya mwalimu ili kupata namba katika kikosi cha kwanza.

“Ni kweli kuna viungo wazuri, mimi najiamini ninaweza ndiyo maana Simba wameniona na kunisajili na nipo tayari kuwatumikia kwa moyo wangu wote ili kuweza kurejesha heshima yake iliyopotea,” alisema Ibrahim.

Tangu 2012 Simba haijawahi kuchukua ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara na ndiyo mara ya mwisho kushiriki michuano ya kimataifa.

Walter Zenga Kuziba Nafasi Ya Ronald Koeman
Video: Wabunge Upinzani watoka Bungeni wakiwa wamejifunga plasta mdomoni