Moja kati ya wapinzani wakuu wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda katika kinyanyiro cha Uchaguzi Mkuu, Dk. Kizza Besigye amekamatwa leo na jeshi la polisi nchini humo ikiwa ni siku mbili kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu.

Taarifa kutoka nchini humo zimeeleza kuwa Dk. Besigye alikamatwa na Polisi katika jiji la Kampala akiwa ameongozana na mamia ya wafuasi wake waliofunga barabara kadhaa.

Jeshi la Polisi lilifyatua mabomu ya machozi na kuwatawanya wafuasi wake kisha kumtia mbaroni mwanasiasa huyo ambaye alishikiliwa kwa saa kadhaa kwa mahojiano na kisha kuachiwa.

Besigye

Polisi wameileza BBC kuwa Mgombea huyo alikamatwa kwa kuwa alikaidi agizo la Jeshi la Polisi kuhusu barabara walizompangia kupita, na badala yake alipita barabara ya Mukwana na kusababisha msongamano mkubwa usiokuwa na usalama.

Dk. Besigye ni kati ya wagombea nane wanaogombea urais wa nchi hiyo. Aliwahi kuwa Daktari wa Museveni kwa muda mrefu na baadae aligeuka kuwa mpinzani wake akidai kuwa kiongozi huyo ni ‘Dikteta’.

Picha, Orodha Kamili ya Washindi wa Tuzo za Grammy 2016
Rais Magufuli awateua Mabalozi wapya, awapandisha vyeo Polisi na kuwapangia kazi mpya