Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko ameziagiza Kampuni za usambazaji Mbolea ya ruzuku Mkoani humo, kuhakikisha mbolea inawafikia mawakala badala ya kuificha kwenye maghala yao.
Mrindoko ametoa maagizo hayo mara baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika baadhi ya maghala ya makampuni hayo Manispaa ya Mpanda na kushuhudia shehena kubwa ya mbolea imerundikwa badala ya kuwa kwa mawakala.
Akiwa katika ghala la Kampuni ya mbolea ya Yara, Mrindoko ameambiwa kuwa sababu inayofanya mbolea kutokwenda kwa mawakala ni kutokana na serikali kufanya malipo hivyo mawakala kuzidiwa na madeni.
Kufuatia maelezo hayo, Mrindoko akaagiza wasimamizi wa kampuni hiyo na kampuni zingine zilizoidhinishwa kusambaza mbolea mkoani humo kuhakikisha mbolea inawafikia wakulima vinginevyo ataamuru jeshi kuingia kwenye maghala hayo kusambaza mbolea wenyewe.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewataka mawakala wa mbolea ya Ruzuku mkoani humo kuwafikia wakulima katika maeneo waliyojiandikishia ili kuwapunguzia adha ya kufuata mbolea mjini Mpanda.
Aidha, pia Mrindoko amewaagiza Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanasimamia zoezi hilo ili azma ya Serikali ya kuweka ruzuku kwenye mbolea iweze kuonekana.